SHARE

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imefuta maombi ya kesi ya kikatiba yaliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kutupwa kwa kesi hiyo kumetokana na mahakama hiyo kukubali pingamizi la walalamikiwa kwamba mahakama hiyo haina mamkala ya kuyasikiliza.

Walalamikiwa katika maombi hayo ni  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (kwa sasa Paul Makonda), Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (Simon Siro) na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) (Camillius Wambura).

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo  la majaji watatu, likiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Sekiet Kihiyo, akisaidiana na Pellagia Khaday na Dk. Lugano Mwandambo.

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo, Jaji Khaday alisema upande wa walalamikiwa uliwasilisha pingamizi la awali kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa sababu mlalamikaji alitakiwa kuwasilisha katika mamlaka husika.

Pia sheria za haki za msingi kifungu cha 8 kidogo cha (2) sura ya 3, inakataza mahakama hiyo kusikiliza maombi kama hayo na kwamba kuna mamlaka zinazoshughulikia kabla ya kufikishwa mahakamani kwa sababu si kesi ya kikatiba.

Aidha, mahakama imetoa uamuzi huo baada ya mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani kuwasilisha majibu ya pingamizi la awali la walalamikiwa hata baada ya kupewa muda wa kufanya hivyo.

Katika kesi ya Msingi ya Kikatiba Mbowe alikuwa anapinga kitendo cha polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.

Mbowe katika kesi hiyo alidai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu, yako kinyume cha katiba kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha.

Kutokana na madai hayo, Mbowe alidai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.

Kadhalika alidai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo, hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi na kwamba mahakama kama itaona alikuwa sawa kutoa amri hiyo, imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here