SHARE

Maelfu ya akina mama wanaendelea kunufaika na huduma ya ujumbe mfupi wa maandishi unaotolewa bure na Vodacom Tanzania Foundation wa ‘Wazazi Nipendeni’, unazidi kuendelea kuwanufaisha maelfu ya akina mama wajawazito kupitia dondoo mbali mbali za kiafya.

Akiongea na mtandao huu Faidha Abdallah pichani ambaye ni mkazi wa Buguruni jijini Dar es Salaam anasema amekuwa akitumia huduma hiyo ambayo imekuwa msaada mkubwa kwake.

“Kupitia huduma hii ninaweza kujifunza namna ya uzazi salama kupitia simu yangu ya kiganjani bila malipo yoyote. Nimekuwa nikipokea ujumbe kila wiki na ninaishukuru  Vodacom Tanzania Foundation pamoja na wadau wengine waliofanikisha huduma hii nzuri,” anasema.

“Pamoja na kuwa nimezaa na kukuza watoto wawili, sikufahamu kuwa kumbe ni muhimu sana kumnyonyesha mtoto kwa miezi sita bila kumkatisha kabla ya kuanza kumlisha aina nyingine ya chakula,” anaelezea

Naye Meneja Ruzuku na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald alisema jijini Dar es Salaam kuwa, zaidi ya wateja milioni moja wamejiunga na huduma hiyo tangu izinduliwe mwaka 2012.

“Wateja waliojiunga na huduma hii wamepokea jumla ya ujumbe mfupi unaofikia milioni 55 wenye maelekezo mbali mbali  juu ya afya bila malipo. Ujumbe wanaopokea ni pamoja na kubaini dalili hatari kwa uja uzito mapema, maendeleo ya mtoto, namna ya kuepuka maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa  mtoto, vyakula muhimu kwa mama mja mzito, uhuhimu wa  mama kuhudhuria kliniki mapema,” anaeleza

Oswald  anasema, kupitia ujumbe mfupi akina mama wajawazito wanaelimishwa namna ya kuishi wakiwa na afya ili waweze kujifungua watoto wenye afya bora pia watu wengine kama vijana, akina mama na wazee wanaweza kujifunza namna ya kujikinga na magonjwa mbali mbali kama Malaria na mengineyo.

Wateja wetu  wanaweza kupata   huduma hii ya bure kwa kutuma ujumbe kwenye namba 15001 au 15012 na wataweza kupokea ujumbe mfupi kupitia simu zao za viganjani.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here