SHARE

Gazeti la Uturuki la Yeni Akit limemtaja Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud wa Saudia kuwa ni mtu hatari sana kwa kueneza fitina baina ya nchi za Kiislamu.

Gazeti hilo limenukuu tuhuma za kipropaganda zinazofanywa na nchi zilizokata mahusiano na Qatar kumlenga Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki, kufuatia hatua ya serikali ya Ankara kupinga uamuzi huo wa Saudia.  Yeni Akit sambamba na kuzitaja nchi hizo za Kiarabu kwa jina la ‘midoli ya shetani mkubwa’ limemtaja Mfalme Salman bin Abdulaziz Aal Saud kuwa kiongozi wa mkuu wa waenezaji fitna baina ya nchi za Kiislamu.

Viongozi wa Misri na Saudia wakiweka mikono yao na Trumpo mjini Riyadh

Aidha gazeti la Yeni Akit limemtaja Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri kuwa kinara wa mapinduzi ya kijeshi, sambamba na kuielezea hatua ya serikali ya Cairo ya kushirikiana na Saudia katka kukata uhusiano wake na Qatar kuwa ni ‘hatua ya kibaraka.’ Itakumbukwa kuwa Saudia, Misri, Bahrain na Imarata zilitangaza kukata mahusiano yao na serikali ya Doha, kwa tuhuma kuwa Qatar inaunga mkono harakati mbili za Kiislamu za Palestina HAMAS na Ikhwanul Muslimin ya nchini Misri. Wakati huo huo makundi kadhaa ya wanamapambano  ya Palestina yamekosoa vikali matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir aliyedai kuwa harakati ya Kiislamu ya Palestina ‘HAMAS’ kuwa eti ni ya kigaidi.

Hali ya uhasama wa Saudia na Qatar

Taarifa iliyotolewa na makundi hayo ya Kipalestina mapema leo imesema kuwa, matamshi ya waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Saudia hayana lengo jingine ghairi ya kuuridhisha utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na washirika wake. Jumanne iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir sambamba na kudai kuwa harakati hiyo ya HAMAS ni ya kigaidi, alilaani uungaji mkono wa Qatar kwa harakati hiyo sambamba na kuchukua hatua kali ya kukata mahusiano na Doha.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here