SHARE

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema atakubali matokeo na kukabidhi madaraka kwa amani ikiwa atashindwa katika Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika nchini humo Agosti 8 mwaka huu.

Kenyatta ambaye anawania urais kwa muhula wa pili amewataka wapinzani wake pia kuwa tayari kuyakubali matokeo, ikiwa yatakwenda kinyume na matarajio yao.

“Nawahakikishia Wakenya kuwa nimejitolea kuhakikisha kuwa nchi hii inakuwa na amani. Ikiwa mtaniambia tarehe 8 kuwa mnataka uongozi mpya, kwa unyenyekevu mkubwa nitakubali na kuondoka,” amesema Rais Kenyatta.

Aidha, amewataka wanasiasa kuacha kuwatisha Makamishena wa Tume ya Uchaguzi na badala yake wawape nafasi ya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Naye mgombea wa muungano wa upinzani NASA Raila Odinga akizungumza katika kongamano kuhusu maandalizi ya uchaguzi jijini Nairobi, amemshutumu Rais Kenyatta kwa kutumia fedha za umma na wafanyikazi wa serikali kuendeleza kampeni zake, kinyume na sheria.

Ameishtumu Tume ya Uchaguzi kwa kusalia kimya kuhusu suala hili  na kuongeza kuwa, kinachoendelea kinatia doa na kuzua wasiwasi ikiwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki.

Wakati huo huo, amesema mkataba wa kuipa kampuni moja ya Dubai kazi ya kuchapisha makaratasi ya kupigia kura haikufanywa kwa wazi, lakini pia ameihusisha na viongozi wa juu wa serikali kuonesha kuwa inaingilia uchaguzi huo.

Odinga na Kenyatta wanarudiana tena katika uchaguzi unaotabiriwa kuwa na ushindani mkubwa.

Mwaka 2013, wawili hao walichuana na Uhuru kutangazwa mshindi, matokeo ambayo Odinga alipinga hata baada ya kwenda katika Mahakama ya juu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here