SHARE

KATIKATI ya mvutano baina yake na Serikali, kampuni ya migodi ya Acacia imetangaza neema kwa wahitimu wa fani mbalimbali wa ngazi ya vyuo vikuu nchini.

Majadiliano kati ya kampuni mama ya Acacia ya Barrick Gold na kamati maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli yalianza jijini mwishoni mwa mwezi uliopita kutatua mvutano wa malipo ya Sh. trilioni 425 ambazo Acacia inadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mujibu wa tangazo la Acacia lililotoka katika gazeti dada la The Guradian la jana, Acacia imefungua ‘Mpango wa Tukue Pamoja kwa Wahitimu wa Shahada’.

Mpango huo, kwa mujibu wa tangazo hilo, ni wa miaka miwili ambao utawawezesha wahitimu hao kuja kuwa waajiriwa na Acacia.

Kada za wahitimu wa vyuo vikuu zinazotakiwa ili kukua pamoja na Acacia, kwa mujibu wa tangazo hilo, ni Uhandisi Migodi, Uchenjuaji Madini na Miamba.

Kada zingine ni Mazingira, Utafiti wa Madini, Utunzaji, Upimaji, Ununuzi, Elimu, Fedha, Utawala, Mazingira, Sayansi ya Afya na Uhifadhi Jamii.

Wahitimu hao ambao wametakiwa kuwa wenye ari, msukumo na kujitambua wenyewe watakaobahatika kuchukuliwa na Acacia, kwa mujibu wa tangazo hilo, watajiunga na waajiriwa wa kampuni hiyo migodini ili kufanyiwa tathmini na kupata uzoefu kwanza kwa faida ya mhitimu na kampuni.

Tangazo lilisema baada ya miaka miwili, wahitimu wanaweza kuajiriwa kwa masharti ya kudumu na kufikiriwa kupanda ngazi mbalimbali ndani ya kampuni.

“Kila nafasi itakuwa na mshahara mnono, ambao utajumuisha masurufu na mazingira mazuri ya likizo,” tangazo hilo limesema likiweka ukomo wa umri na tarehe ya kuomba nafasi hizo.

TUME MBILI
Acacia inayomiliki migodi mitatu ya dhahabu nchini ilitoa taarifa mwishoni mwa mwezi uliopita ikieleza kuwa imepokea kutoka TRA hati ya madai ya jumla ya Sh. trilioni 425.

Taarifa hiyo ilisema TRA ilionyesha katika madai yake kuwa mgodi wa Acacia wa Bulyanhulu unadaiwa kodi ya tangu mwaka 2000 na Pangea unadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.

Taarifa ya TRA kwa Acacia ilifuatia ripoti ya tume mbili za Rais Magufuli ambazo Mei na Juni, mwaka huu ziligundua udanganyifu mkubwa katika biashara ya makinikia ya Acacia.

Moja ya ripoti hizo ilionyesha kuwa nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.

Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa sh. trilioni 108 na kamati ya wachumi na wanasheria iliyoongozwa na Prof. Aidan Osoro wa Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wakati kamati ya Tanzania katika mazungumzo hayo inaongozwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, kamati ya Barrick Gold inaongozwa na Afisa Mwendeshaji Mkuu, Richard Williams.

Uchambuzi uliofanywa na TRA, kwa mujibu wa taarifa ya Acacia, ulionyesha kuwa mgodi wake wa Bulyanhulu unadaiwa na mamlaka Sh. trilioni 344.8 na mgodi wa Pangea Sh. trilioni 76.1.

Hivyo madai hayo ya TRA yalionyesha kuwa Acacia inadaiwa Sh. trilioni 89.5 ikiwa ni malimbikizo ya kodi na Sh. trilioni 335.9 za adhabu na riba.

WAKATI MGUMU

Acacia ilikuwa katika wakati mgumu hata kabla ya ripoti ya Prof Osoro ya Juni 24, baada ya kamati ya kwanza iliyoteuliwa na Rais Magufuli Machi 29, ikiwa na wajumbe nane wenye taaluma za jiolojia, kemia, uhandisi kemikali na uhandisi uchenjuaji madini, kuchunguza kiwango cha madini kwenye makontena yenye makinikia kuonyesha kuwapo kwa udanganyifu.

Acacia ilikuwa msafirishaji mkuu wa makinikia nchini kabla ya Rais Magufuli kuagiza kusimamishwa Februari, mwaka huu.

Kamati hiyo maalumu ilikuwa chini ya uenyekiti wa Profesa wa masuala ya miamba, Abdulkarim Mruma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Rais Magufuli alizuia makontena 277 ya makinikia ya Acacia yaliyokuwa yanasafirishwa kwenda kuchenjuliwa ughaibuni Machi 23, kisha akaunda kamati hizo mbili kufuatilia kilichokuwamo baada ya kuwapo kwa hisia za udanganyifu wa kiasi halisi cha madini kilichomo kwenye mchanga huo.

Baada ya kamati ya kwanza kumkabidhi ripoti ya uchunguzi Mei 24, Rais Magufuli alichukua uamuzi wa kusitisha upelekaji mchanga nje ya nchi mpaka itakapoelezwa vinginevyo baadaye.

Aidha, Rais Magufuli aliwawajibisha baadhi ya watendaji wa serikali ikiwamo kutengua uteuzi wa Prof. Sospeter Muhongo kama Waziri wa Nishati na Madini.

Pia miongoni mwa mapendekezo ya kamati ya Prof Osoro ni kupiga marufuku usafirishaji mchanga nje na kujenga kiwanda cha kuchenjua makanikia hapa nchini, jambo ambalo Rais Magufuli alilikubali papo hapo na Barick Gold, sasa, imeahidi kusaidia kufanikisha.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here