SHARE

MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya Bodi ya Wadhamini wa Chama Cha Wananchi CUF inayomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif ya kutaka Msajili wa Vyama vya Siasa asitoe ruzuku kwa CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Maombi hayo namba 21 ya mwaka 2017 yametupiliwa mbali na Jaji Wilfred Ndyansobera, baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata anayemuwakilisha mdaiwa wa pili Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kudai kesi imeitishwa kwa ajili ya uamuzi.

Katika uamuzi wa maombi hayo, ambayo mdaiwa wa kwanza ni Prof. Lipumba, Jaji Ndyansobera amesema anakubaliana na moja kati ya pingamizi la (AG) kwamba vifungu vya sheria vilivyotumika kufungua shauri hilo sio sahihi.

Aidha, alisema anakubaliana na hoja za Bodi hiyo (upande Maalim Seif) kwamba suala la Bodi hiyo kutokuwa na uhalali linahitaji ushahidi wa kina.

Pia kuhusu suala la Maalim Seif kusaini hati mbalimbali za shauri hilo bila kupewa mamlaka, Jaji Ndyansobera alisema hilo sio pingamizi kwani mahakama haiwezi kutoa uamuzi kwa kuangalia kiapo tu.

“Hivyo mahakama imetupilia mbali maombi hayo, kwa sababu sheria iliyotumiwa kufungua maombi hayo sio sahihi, lakini waombaji wanaweza kukata rufaa ama kufungua kesi nyingine,” alisema Jaji Ndyansobera.

Baada ya kuelezwa hayo, upande wa Maalim ulisema utafungua upya kesi hiyo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here