SHARE

Polisi mkoani Singida wanamshikilia Mbunge Manyoni (CCM), Daniel Mtuka (51) kwa tuhuma ya kumgonga kwa gari mwanafunzi wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Sukamahela, Salome Paschal (10) na kusababisha kifo chake papo hapo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magilingimba alisema ajali hiyo ilitokea jana katika Kijiji cha Sukamahela, Kilimatinde wilayani Manyoni.

Alisema mbunge huyo alikuwa akirejea jimboni mwake akitokea Dodoma akiendesha gari lake aina ya Toyota Prado na alimgonga mwanafunzi huyo aliyekuwa akivuka kutoka upande wa kulia kwenda kushoto mwa barabara.

Kamanda huyo alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva Mtuka, kushindwa kuchukua tahadhari kwa watumiaji wengine wa barabara.

“Anashikiliwa na baada ya mahojiano, atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayomkabili,” alisema Kamanda Magilingimba na kuongeza, “Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kwa uchunguzi wa daktari na baada ya hapo, utakabidhiwa kwa ndugu kwa hatua za mazishi.”

Katika hatua nyingine, Kamanda Debora alisema watu wawili akiwamo Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Ngara mkoani Kigoma, Alfred Kafuku wamefariki dunia papo hapo, baada gari walilokuwa wakisafiria kugonga lori aina ya DAF kwa nyuma.

Alimtaja mwingine aliyefariki kuwa ni dereva wa gari hilo anayedhaniwa kuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ambaye hata hivyo, utambulisho wake haukujulikana mara moja.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here