SHARE

Nyota njema imeanza kuiwakia klabu ya Simba baada ya jioni kutwaa Ngao ya Jamii, kwa kuwafunga wapinzani wao Yanga kwa penalty 5-4, baada ya kutoka sare katika muda wa kawaida.

Penalti ya Juma Mahadhi, ndiyo iliyovuruga kiwango bora kilichoonyeshwa na kikosi cha Yanga na kuwaweka kimya kwa sehemu kubwa mashabiki wa Simba ambao walikuwa wamejazana kwa wingi uwanja wa Taifa Dar es Salaa.

Kiungo mpya wa Yanga Papy Kabamba Tshishimbi ndiyo alikuwa kivutio kikubwa kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa na kuwafunika Haruna Niyonzima pamoja na Emmanuel Okwi wa Simba.

 Makipa wote wawili walionyesha uwezo mkubwa na kuokoa mikwaju ya penati tano za kwanza kabla ya Mahadhi kupaisha juu penalti ya niongeza baada ya zile tano za awali kumalizika timu zote zikipata mikwaju minne na kukosa mmoja.

Katika kipindi cha kwanza Yanga iliweza kuutawala mchezo na kupiga mashuti mawili langoni mwa Simba wakati Simba iliweza kupiga shuti moja ambalo lilidakwa na kipa Youth Rostand.

Timu zote mbili ziliweza kumaliza kipindi cha kwanza zikiwa zimepata kona tatu kila upande wakati Yanga walifika mara nne kwenye lango la Simba wakati Simba walifanya hivyo mara tatu.

Katika mchezo wa leo, uliochezeshwa na marefa wa Dar es Salaam Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Ferdinand Chacha wa Mwanza, timu zilishambuliana kwa zamu ndani ya dakika 90 za kawaida.

Lakini sifa ziende kwa safu za ulinzi za timu zote, Yanga ikiongozwa na Yondani na Simba ikiongozwa na Mwanjali pamoja na makipa wao, Manula na Rostand.

Safu ya ulinzi ya Yanga leo ilikuwa ina uhai zaidi kutokana na uhodari na ufundi wa kiungo mpya wa ulinzi, Mkongo Papy Kabamba Tshishimbi aliyesajiliwa kutoka Mbabane Swallows ya Swaziland.

Donald Ngoma aliisumbua ngome ya Simba, lakini akapoteza nafasi mbili nzuri za kufunga kama ilivyokuwa kwa Okwi, naye alipoteza nafasi moja nzuri. Winga Emmanuel Martin alikaribia kuifungia Yanga kipindi cha pili baada ya kuwatoka mabeki wa Simba na kuingia na mpira kwenye boksi, kabla ya kupigiwa filimbi ya kuotea na refa Sasii. Beki mpya wa Yanga, Gardiel Michael leo alimdhibiti vizuri Kichuya.

Baada ya mchezo huo, Simba walikabidhiwa Ngao na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku Medali wakivishwa na Makamu wa Rais, Michael Wambura.

Mzimbabwe, Method Mwanjali, Emmanuel Okwi,Haruna Niyonzima, na wazawa Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim ‘Mo’ ndiyo waliopata penalti wakati Mohamed Tshabalala ndiye aliyekosa.

Yanga waliopata ni Papy Tshishimbi, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Ibrahim Ajibu waliokosa ni Kelvin Yondani na Juma Mahadhi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here