SHARE

ASKARI wa kituo kikuu cha polisi mjini Bukoba, Koplo Mussa Msanya (44), amekutwa amekufa na mwili wake ukielea katika maji katika Ziwa Victoria saa chache baada ya kumtajia mkewe namba za siri za sanduku la mkononi lililokuwa na namba ya siri ya kadi ya ATM ndani yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema jana, kuwa mwili huo umeopolewa katika ufukwe ulioko eneo la Kiloyera, Manispaa ya Bukoba na kwamba chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana.

Kamanda Ollomi alisema Jumamosi iliyopita mke wa marehemu, Halima Mussa, alifika kituo kikuu cha polisi saa sita mchana na kutoa taarifa kuwa ana wasiwasi na usalama wa mume wake.

“Huyo mama alidai alipoamka alikuta karatasi iliyoandikwa namba ya siri ya sanduku dogo ambalo askari huyo alikuwa akitunzia nyaraka zake za siri, akashtuka,” alisema Ollomi.

Alisema baada ya kusoma namba hizo mama huyo alifungua sanduku hilo na kukuta namba ya siri ya akaunti ya benki na kadi ya benki ya kutolea pesa (ATM) na simu mbili za mkononi.

“Mkewe amedai hakukuwa na ujumbe mwingine wowote katika sanduku hilo hali iliyozidisha wasiwasi, maana awali alidhani mume wake yuko kazini kutokana na askari huyo kuondoka nyumbani akiwa amevalia sare ya Jeshi la Polisi,” alisema kamanda Ollomi.

Kutokana na taarifa hizo, alisema polisi walianza kufanya uchunguzi na juzi saa 10:45 jioni, walipata taarifa kutoka kwa wafanyabiashara wa samaki kuwa wameona mwili wa mtu aliyevaa sare za polisi ukielea.

Alisema polisi kwa kushirikiana na wafanyabiashara hao waliuopoa mwili wa askari huyo na kuupeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera kwa ajili ya uchunguzi.

Kamanda Ollomi alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mwili wake haukuwa na kovu lolote, zaidi ya kuvimba tu kutokana na kufa maji.

Alisema wanasubiri taarifa za kitabibu kutoka kwa madaktari na hapo ndipo itajulikana chanzo cha kifo hicho na kwamba baada ya uchunguzi, mwili utasafirishwa kwenda Kigoma kwa mazishi.

Kamanda Ollomi alisema askari huyo ametumikia jeshi kwa miaka 18.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here