SHARE

Baada ya kushadidi vitendo vya ukatili na mauaji dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa Myanmar na kulazimika maelfu miongoni mwao kuwa wakimbizi, serikali ya Bangladesh imetangaza kwamba, inakusudia kuwahamishia wakimbizi hao Waislamu katika kisiwa kimoja cha nchi hiyo katika Ghuba ya Bengal na hivyo kuwapatia makazi ya muda huko.

Hossain Toufique Imam, mshauri wa kisiasa wa Sheikh Hasina, Waziri Mkuu wa Bangladesh amesema kuwa, haiwezekani kuzuia kuingia nchini humo Waislamu wa Rohingya wanaokimbia dhulma na ukandamizaji wa serikali ya Myanmar.

Hossain Toufique Imam ameongeza kuwa, serikali ya Dhaka imezitaka asasi za kimataifa ziandae mazingira ya makazi ya muda katika kisiwa cha Thengar Char kwa ajili ya wakimbizi wa Kirohingya. Kabla ya hapo pia, serikali ya Bangladesh iilikuwa imezungumzia mpango wake wa kuwapatia makazi ya muda wakimbizi wa Kirohingya huko katika kisiwa cha mbali cha Thengar Char kilichoko kusini mwa nchi hiyo.

Zaidi ya nyumba 2600 za Waislamu wa Rohingya zimechomwa moto katika jimbo la Rakhine Myanmar

Kisiwa hicho ambacho kilijitokeza takribani miaka 11 iliyopita kinahesabiwa kuwa eneo hatari mno kwa ajili ya kuishi hasa kutokana na kuwa ni ukanda wa mafuriko, kina baridi kali, hakina huduma huku likiwa pia ni eneo la kurandaranda maharamia. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana pendekezo la serikali ya Bangladesh la kuwahamishia Waislamu wakimbizi wa Rohingya katika kisiwa hicho cha mbali likakabiliwa na upinzani mkali wa duru za kieneo na kimataifa.

Hatua ya serikali ya Bangladesh ya kuwafukuza Waislamu wa Rohingya na kuzidi kuwashinikiza inalenga kuzikinaisha asasi za kimataifa ili zitoe msaada wa kuwapatia makazi Waislamu wakimbizi wa Kirohingya huko katika kisiwa cha Thengar Char.

Mkuu wa Ofisi ya Kimataifa ya Uhajiri nchini Bangladesh anasema kuwa: Waislamu wa Rohingya wanakabiliwa na maafa ya kibinadamu hivyo jamii ya kimataifa izingatie na kuguswa na hali ya Waislamu hao na wakati huo huo ni jambo la dharura kuchukuliwa hatua za kuishinikiza serikali ya Myanmar ili ikomeshe mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Waislamu wa Kirohingya walioingia nchini Bangladesh wanakabiliwa na hali mbaya sana.

Wanajeshi wa Myanmar wanatuhumiwa kuhusika na mauaji dhidi ya Waislamu wa Rohingya

Kwa msingi huo basi, duru za kimataifa na jamii za Kiislamu hazikubali kuona serikali ya Bangladesh ikiifanya hali ya Waislamu hao kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.

Hata kama serikali ya Bangladesh inadai kwamba, uwepo wa wakimbizi hao wa Kiislamu wa Rohingya kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar unaisababishia nchi hiyo matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kiusalama, lakini ufumbuzi wa jambo hilo sio kuwahamishia Waislamu hao madhlumu katika kisiwa cha mbali ambacho hakuna asasi yoyote ile ya kimataifa inayothibitisha juu ya uwezekano wa binadamu kuishi katika kisiwa hicho.

Gazeti la The Independent la nchini Uingereza linaripoti kwamba:

Idadi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wamekuwa wakikimbilia nchini Bangladesh kutokana na kushadidi hujuma na mauaji dhidi yao katika siku za hivi karibuni imeongezeka licha ya kuwa wanajua kwamba, mwisho wa safari hiyo haufahamiki.

Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wa Myanmar ambao wamekuwa wakishambulia na kuwaua Waislamu wa Rohingya

Vyovyote itakavyokuwa, Bangladesh ikiwa na lengo la kuwapatia makazi wakimbizi wa jamii ya Kiislamu ya Rohinigya na ikiwa ni nchi ya Kiislamu haipaswi kufanya mambo kwa namna ambayo duru za Magharibi nazo ziutilie alama ya swali mshikamano wa Waislamu na msaada wa Mwislamu kwa ndugu yake Mwislamu; na hivyo zitumie fursa hiyo kuonyesha kwamba, ni duru za Kimagharibi tu na asasi zao za kutetea haki za binadamu ndizo ambazo zinaweza kushughulikia matatizo ya Waislamu hao, ingawa hadi sasa madola ya Magharibi nayo yameamua kunyamazia kimya jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Bila shaka kuishinikiza serikali ya Myanmar ili iwatambue Waislamu wa jamii ya Rohingya wa jimbo la Rakhine kwamba, ni raia wa nchi hiyo ni hatua ambayo inaweza kuwa ufumbuzi wa kimsingi kwa ajili ya kuhitimisha mauaji na umwagaji damu dhidi ya Waislamu hao wasio na hatia.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here