SHARE

Klabu za Simba na Azam FC, leo zimeshindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyopigwa uwanja wa Azam Complex Dar es Salaam.

Matokeo hayo yanaishusha Simba hadi kwenye nafasi ya pili, na timu ya Tanzania Prisons ambayo leo imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Majimaji ya Songea inakaa kileleni mwa msimamo kwa kufikisha pointi sita kufuatia kushinda mechi zote mbili ilizocheza awali.

Wenyeji Azam walijitahidi kupambana ili kuweza kupata pointi tatu nyingine lakini Simba, walisimama imara na kufanikiwa kulazimisha sare hiyo na kuzifanya timu zote mbili kufikisha pointi nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Mshambuliaji John Bocco, leo alirudi nyumbani uwanja wa Azam Complex sambamba na wachezaji Aishi Manula, na Erasto Nyoni na kupata mapokezi mazuri ambayo hata hivyo licha ya kujitahidi kupambana kuipigania Simba lakini haikuwa rahisi mbele ya Agrrey Moris na Yakub Mohamed.

Katika kipindi cha kwanza Simba walitengeneza nafasi tano lakini kipa wa Azam alifanya kazi nzuri ya kuokoa hivyo hivyo kwa Azam waliweza kufika langoni mwa Simba mara nne lakini Manula alifanya kazi yake vizuri.

Mshambuliaji mpya wa Simba raia wa Ghana Nicholaus Gyan, mara kadhaa alijaribu kuwalamba chenga mabeki wa Azam lakini alikutana na ukuta mkali chini ya viungo Stephen Kingue na Himid Mao, ambao walifanya kazi yao vizuri ya kuilinda ngome ya ulinzi.

Pamoja na timu hizo kwenda mapumziko bila kufungana lakini wachezaji wawili wa Azam Himid Mao na Bruce Kagwa walionyeshwa kadi za njano wakati kwa upande wa Simba kiungo Mzamiru Yasini naye akionyeshwa kadi kama hiyo kutokana na mchezo mbaya.

Kipindi cha pili kocha wa Azam alifanya mabadiliko kwa kumtoa Daniel Amoah na kumuingiza Frank Domayo ambaye alizidi kuimarisha eneo la kiungo na kupandisha kwa wingi mipira kwa washambuliaji wao Yahya Mohamed na Mbaraka Yusufu.

Baada ya mambo kuwa magumu kocha Aristica Cioaba, alifanya mabadiliko mengine kwa kumtoa Mbaraka na kumuingiza Ramadhani Singano ambaye aliongeza kasi ya mashambulizi lakini Simba nao waliweza kuwaingiza Said Ndemla na Mohamed Ibrahim walioingia kuchukua nafasi ya Gyan na Shiza Kichuya walisaidia idadi ya mashambulizi lakini walishindwa kubadilisha matokeo ya mchezo huo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here