SHARE

Mshambiliaji wa mabingwa watetetezi wa ligi kuu Tanzania bara Ibrahim Ajibu jana ameipa furaha Yanga baada ya kufunga bao pekee lililoipa timu hiyo pointi tatu walipokuwa wanacheza ugenini dhidi ya Njombe Mji ya Ruvuma.

Bao hilo limeifanya Yanga kufikisha pointi nne sawa na timu ya Simba, lakini mabingwa hao wapo kwenye nafasi ya tano kwenye msimamo huku Mtibwa sugar wakiongoza ligi hiyo kwa tofauti ya point moja tu.

Ajibu alifunga bao hilo mapema dakika ya 16, akipiga mpira wa adhabu ndogo uliompita kipa wa Njombe Mji David Kisu na mpira kujaa wavuni.

Wenyeji Njombe Mji ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi lakini baada ya dakika tano walijikuta wakikaribisha mashambulizi ya Yanga kwenye lango lao na kufungwa bao hilo ambalo lilidumu kwa muda wote wa mchezo.

Mshambuliaji wa Yanga Donald Ngoma alipoteza nafasi ya wazi ya kuifungia timu yake bao la pili kufuatia pasi nzuri ya Gadiel Machael lakini shuti lake lilipaa juu ya lango la Njombe Mji.

Kipindi cha pili kocha wa Njombe Mji Hassani Banyai, alifanya mabadiliko kwa kumtoa  Awadhi Salum ambaye alionekana kushindwa kuisaidia timu yake kwenye eneo la kiungo.

Mbadiliko hayo yalionekana kuiimarisha Njombe na kuanza kuishmbulia sana Yanga lakini walishindwa kutumia vizuri nafasi walizozipata kwenye mchezo huo.

Kipa wa Yanga Rostand alifanya kazi kubwa na yaziada kwenye mchezo huo kwa kuokoa mashambulizi mengi ya wenyeji wao baada ya wachezaji wake kuchoka huku upepo ukiwa ni moja ya sababu iliyowachangia mipira kushindwa kukaa mbele.

Huo ni ushindi wa kwanza kwa Yanga tangu kuanza kwa msimu huu ambapo katika mchezo wa kwanza uliokuwa wa ufunguzi timu hiyo ikiwa nyumbani uwanja wa Uhuru iliweza kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Lipuli ya Iringa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here