SHARE

Mke wa Rais Robert Mugabe, Grace Mugabe ametoa wito unaoweza kuzua balaa baada ya kuwataka vijana kuwafanyia vurugu wanachama wa zamani wa Zanu-PF katika mkutano wa vijana uliohutubiwa na mumewe katika Uwanja wa Bindura, Mashonaland Jumamosi iliyopita.

Mwanamama huyo ambaye mwezi uliopita alitawala vichwa vya habari kwenye vyombo vya habari baada ya kumshambulia mwanamitindo wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 20 alipomwona akiwa na watoto wake wa kiume katika hoteli ya Sandton, alimtaka pia Auxillia ambaye ni mke wa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa kumpiga mwanachama yeyote aliyefukuzwa Zanu- PF akimwona anatoka na mumewe.

Katika mkutano huo Grace alimshutumu Mnangagwa kwa kuchangamana na wanachama wa chama hicho waliofukuzwa.

“Baadhi ya vijana wanasema (Rais) Mugabe sasa ni mzee hivyo arithiwe na Mnangagwa. Vijana hawa wakosaji wakifukuzwa kwa utovu wa nidhamu Mnangagwa atawanyamazia na inatutisha tunapowaona nyumbani kwake. Kwa hiyo mama Mnangagwa, ukiwaona watu hawa waliofukuzwa wakija nyumbani kwako wapige; huo ndio wajibu wa mama anayewajibika, lazima udhibiti nidhamu ya watoto wako pamoja na hawa wanaotembea hovyo ili wafanye mambo mazuri yawapasayo,” alisema Grace.

Kadhalika Grace alihoji utiifu wa Mnangagwa kwa Rais Mugabe. “Ikiwa wewe (Mnangagwa) kwa dhati unamuunga mkono rais basi hupaswi kuchangamana na watu waliofukuzwa kwenye chama. Tunakuona wewe (Mnangagwa) katika picha iliyoandikwa ‘mimi ni bosi’ ukiwa na watu waliofukuzwa kwenye chama nah ii lazima ikome,” alisema Grace.

Taarifa zilizopo zinadai Grace na mama Mnangagwa wanaongoza makundi tofauti ndani ya Zanu-PF yanayowania kumrithi Mugabe.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here