SHARE

Kiongozi wa Nasa Raila Odinga amesema maofisa 12 wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi wametajwa na muungano wao kwamba walihusika na dosari zilizojitokeza katika uchaguzi uliofutwa wa Agosti 8 na kwamba anataka wafukuzwe na wafungwe.

Odinga amewataja maofisa hao 12 wakiwemo makamishna Abdi Guliye na Boya Molu pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu Ezra Chiloba, wasaidizi wake wawili Betty Nyabuto na Marjan Hussein Marjan, lazima waadhibiwe kwa kile Nasa wameeleza ni “kuvuruga utashi wa watu”.

“Wale waliosimamia uchaguzi uliopita lazima watazame uchaguzi ujao wakiwa jela na siyo wakiwa kwenye ofisi za IEBC,” alisema Odinga wakati wa mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za sekretarieti ya Okoa Kenya Lavington leo mchana.

Aliendelea kusema: “Hatuhitaji bora uchaguzi. Tunahitaji uchaguzi uendeshwe na wanaume na wanawake wenye uadilifu, siyo hawa kina Chiloba, Guliye, Kassaits wa dunia hii.”

Maofisa wengine waliotajwa na Odinga ni wakurugenzi Immaculate Kasait (uchaguzi), Praxedes Tororey (sherial), James Muhati (Tehama), na Moses Kipkosgey ambaye ni mshauri wa masuala ya kisheria wa Chiloba.

Vilevile, Nasa imewaingiza maofisa usimamizi uchaguzi Nancy Kariuki (Mombasa), Sidney Namulungu (Kisii), na Silas Rotich (Nakuru).

Jana Jumapili, Odinga aliorodhesha miongoni mwa masharti tisa, kujiuzulu maofisa hao mmoja baadaya ya mwingine kabla ya muungano huo kurejea kwenye sanduku la kura kwa uchaguzi wa marudio.

“Wakenya wanakuja kwenu. Okoa chochote mnachoweza na muondoke. Hakutakuwa na uchaguzi huku ninyi mkiwa ndani ya ofisi,” Odinga aliwaambia maofisa wa Tume.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here