SHARE

MAISHA ya utoto na shuleni kuhusu rais wa sasa wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un yamefichukuliwa ikielezwa kwamba kiongozi huyo alikuwa mtukutu na hakuwa mwerevu darasani.

Siri hizo zimeanikwa na mmoja wa majasusi ambaye ni kiongozi wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Korea Kusini, Nam Sung – woo. Korea Kusini ni nchi hasimu na Korea Kaskazini.

Kwa mujibu wa Nam Sung-woo, kwa kuzingatia maisha hayo ya utotoni ya kiongozi huyo namna pekee ya kuepukana na vituko vyake dhidi ya amani ya dunia ni kumuua.

Anaeleza kwamba tabia ya utukutu si jambo la kubahatisha kwa rais huyo na kwa mfano, kuna wakati katika maisha yake ya ujana “alimshughulikia” rafiki yake wa kike kwa kile kinachoelezwa kuwa ‘kosa’ la kumshawishi mpenzi wake huyo kuacha kuvuta sigara.

Nam anasema: “Nilishitushwa pale niliposhuhudia namna Kim alivyokuwa akimporomoshea matusi mpenzi wake kupitia simu baada ya mpenzi wake huyo kumtaka aachane na tabi ya kuvuta sigara mara kwa mara. Tabia hiyo mbaya iliyojaa utukutu ilinifanya niamini kwamba mambo yatakuwa magumu kwa taifa pale kijana huyo atakapokuwa kiongozi mkuu.”

Anaeleza kwamba kama Kim hatauwawa basi vitisho vyake dhidi ya amani ya dunia vitaendelea kushika kasi.

Nam Sung-woo anasisitiza kuwa tabia yake ya utukutu akiwa mdogo ni kama imevuka mipaka sasa.

Kwa muda mrefu sasa ni mambo machache tu yamekuwa yakifahamika kuhusu maisha binafsi ya rais huyo kabla ya kuwa kiongozi mkuu wa taifa lake licha ya kuwapo kwa juhudi za watu mbalimbali ‘kupekua’ historia yake.

Kati ya mambo yaliyogundulika hivi karibuni ni kiongozi huyo kusoma katika shule moja ya bweni nchini Switzerland, na kisha kuondoka bila hata kuhitimu.

Rekodi zinabainisha ya kuwa akiwa amepata kutumia jina bandia Kim alifanikiwa kuwa rafiki wa Joao Micaelo, mtoto wa kiume wa mwanadiplomasia mmoja wa Ureno.

Micaeolo anakumbuka mambo yalivyokuwa wakiwa shuleni pamoja na Kim, akisema hawakuwa werevu sana darasani na wala Kim binafsi hakuwa na dalili zozote zilizoashiria ipo siku atakuwa mkuu wa nchi yake.

Micaeolo anasema: “Hatukuwa ‘vilaza’ sana darasani ingawa pia hatukuwa werevu sana.”

Anaweka bayana kwamba Kim alikuwa akipenda zaidi michezo kuliko masomo ya darasani, na hapo ndipo anapojikuta katika urafiki na mchezaji nyota wa mpira wa kikapu wa zamani wa Marekani Dennis Rodman.

“Aliondoka zake shuleni bila hata kupata matokeo ya mtihani wala hakuhitimu. Alikuwa akivutiwa zaidi na mchezo wa mpira wa miguu pamoja na mpira wa mikono kuliko hata masomo ya darasani,” anaeleza

Lakini mwanafunzi mwingine aliyepata kusoma pamoja na rais huyo anaeleza kwamba mwenzake huyo darasani alikuwa mtu wa kawaida tu.

“Ilikuwa mwaka 1993 alipoingia shuleni. Alikuwa na Kiingereza kibovu kwa mara ya kwanza. Lafudhi yake ilikuwa tata na ilibidi afunzwe katika vipindi vya ziada. Alijifunza pia Kijerumani … na alijitahidi kwa kadiri alivyoweza. Alimudu kuboresha kiwango chake cha Kiingereza lakini akashindwa katika Kijerumani.

“Alikuwa anamudu hisabati. Hakuwa na uwezo mkubwa katika masomo mengine. Tulimpachika jina la utani la Dim Jong-un. Siku moja alitoweka tu hivi, hakuonekana tena,” anaeleza

Inaelezwa kwamba Kim aliachishwa shule baada ya baba yake Kim Jong-il kuhisi kwamba mwanawe huyo ameanza kuvutiwa zaidi na utamaduni wa Marekani.

Micaelo anasema: “Katika maisha yake ya shule bwenini alikuwa na kila kitu kilichohitajika kwa ajili ya burudani, wanafunzi wengine wengi hatukumudu hayo. Huyu alikuwa na televisheni, rekoda ya video, seti ya muziki, mpishi, dereva na mwalimu binafsi.

“Baada ya masomo tulikuwa tukikutana uwanjani kwa ajili ya mchezo wa mpira wa mikono, sote tukiigiza kuwa kama Michael Jordan. Tulikuwa tukivutiwa sana na mchezaji huyo nyota wa Marekani.”

Kwa sasa unaweza kusema Kim amejiondoa katika mausala ya michezo na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa kinu cha nyuklia kiasi cha kuibua mvutano mkali kati ya taifa lake na Marekani, na tayari amekwishafanya majaribio yasiyopungua sita ya kinyuklia na kuzua taharuki kuhusu amani ya dunia.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here