SHARE

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu ameomba marehemu diwani wa viti maalumu, Ester Mpwiniza akamuombee kwa Mola Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ili apone haraka.

Lissu ambaye pia ni mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.

Sugu amesema hayo leo Jumatatu jioni akieleza wasifu wa Mpwiniza aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) Mbeya Mjini kabla ya maziko yaliyofanyika kwenye makaburi ya Sabasaba jijini hapa.

Mbunge huyu amesema anakipeleka kilio hicho kwa Mungu kwa kuwa hali ya nchi ilipofikia sasa si salama kwa kuwa upinzani umekuwa ukipata vikwazo vingi hata pale wanapofanya maombi ya pamoja, kujiombea na kuiombea nchi amani wanazuiwa. Amesema diwani Mpwiniza alikuwa ngao katika ulingo wa kisiasa.

Sugu amesema anaamini Mbinguni aendako Mpwiniza atapokelewa na malaika kutokana na kuyaishi maisha ya upendo, ujasiri na kuwa mwanamke aliyethubutu kuwaunganisha wenzake.

“Nakuomba dada yangu Ester, naamini huko Mbinguni umekwishapokewa na malaika. Nakuomba dada nenda kwa Mungu muombe asimamie uhai wa Tundu Lissu, amlinde na aponye haraka majeraha yaliyosababishwa na shambulio la risasi, Mungu akuongoze kwenye sala,” amesema Sugu.

Sugu pia alitoa sifa kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliyehudhuria msiba huo bila kujali itikadi ya chama chake cha siasa cha CCM na kuonyesha dhahiri alivyo na mapenzi na ndugu zake wa Mkoa wa Mbeya.

Amesema naibu spika ameonyesha ukomavu wa kisiasa na kwamba, hizo ni salamu tosha za kuzipeleka kwenye mamlaka nyingine ambazo badala ya kuwaunganisha wananchi katika misiba kunasababisha wengine waogope kuzikana wakati kifo hakina itikadi.

Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee amesema msiba huo uwe kiunganishi kwa wanawake wote wa chama hicho, akiamini kuwa heri wafao kwa magonjwa yaliyopangwa na Mungu kuliko uwepo wa binadamu wachache wanaotumiwa kutoa roho za wenzao wasiokuwa na hatia.

“Hapa tulipofikia tuseme panatosha, huyo mama leo hii tunakwenda kumpumzisha akiwa na sifa zote, kifo chake hakikupangwa na binadamu lakini wapo hawa wachache wasiojulikana wanaotumiwa kuwaua wenzao kama walivyokusudia kutaka kukatisha uhai wa Lissu,” amesema Mdee.

Naibu Spika, Dk Tulia amesema msiba huo unatoa mafundisho ya kuwaunganisha wana Mbeya na Watanzania wote wapenda amani.

Dk Tulia amesema msiba huo umemgusa ndiyo maana amefika kutoa pole. Ametoa ubani Sh300,000, huku Mbunge Sugu akitoa msaada wa Sh200,000 kwa familia ya marehemu kwa ajili ya kununua saruji ili kumalizia ujenzi wa nyumba iliyopo eneo la Iyela jijini Mbeya.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here