SHARE

Mahakama ya Juu imeitupia lawama Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa kusababisha kufutwa matokeo ya uchaguzi wa rais uliofanyika Agosti 8, mwaka huu.

Katika maelezo ya kina kuhusu sababu za matokeo hayo kufutwa Septemba Mosi, Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu alifichua namna IEBC ilivyoudhi na kukaidi maelekezo iliyopewa na Mahakama ya Juu kufungua kompyuta ili kuthibitisha mfumo wa kuhifadhi takwimu baada ya upinzani kulalamika kwamba ulidukuliwa.

Mwilu alisema mfumo wa Tehama wa IEBC uliingiliwa na ukachezewa na takwimu zilizomo zikabadilishwa.

“Mfumo mzima umechezewa na umechafuliwa au IEBC iliingilia takwimu na ilikana kuwa mfumo wake uliingiliwa,” alisema.

“Amri tuliyotoa ufanyike uchunguzi ilikuwa fursa pekee adhimu kwa IEBC kuwathibitisha uongo wa waliofungua kesi lakini IEBC haikutii amri ya mahakama.”

Mwilu aliongeza kwamba tume hiyo “mara kwa mara” haikutii amri hali aliyosema ilifikia “kiwango cha juu”.

“IEBC ilipaswa kuwa na mfumo wa usaidizi. Tuliwapa walalamikaji fursa ya kusoma tu lakini kulikuwa na ukaidi wa wazi kwa upande wa IEBC kwamba hawakutaka kutoa taarifa kwa ukamilifu.”

Kisha aliongeza maswali kuhusu uhalali wa kura zilizoongezeka kwa uchaguzi wa urais tu ikilinganishwa na wengine hayakujibiwa kikamilifu.

Aidha, Jaji Isaac Lenaola, mmoja wa majaji watano waliounga mkono kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa rais alisema mahakama imechunguza na kubaini “ukiukwaji wa misingi iliyowekwa na katiba na sheria za uchaguzi kama walivyolalamika waliofungua kesi.”

“Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipuuza sheria na katiba katika kiwango ambacho wao walijifanya kuwa sheria. Kwa upande wetu, chaguzi si tukio moja bali mchakato mzima, na hii imeelezwa vizuri katika vitabu vya IEBC,” alisema Lenaola.

Alisema Wakenya walipoteza Imani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 kutokana na vurugu na mkanganyiko katika namna ya kuhesabu kura na kutangaza na kuondokana na hali hiyo ndipo Kriegler alipendekeza matumizi ya teknolojia.

Lenaola alisema mfumo wa teknolojia unaotumiwa unapaswa kuwa wazi na unaohakikiwa.

“IEBC ilishindwa kuhakiki matokeo ambayo yalitumwa kwa mfumo wa kielktroniki kutoka vituoni kabla ya kutangaza jambo ambalo lilikuwa ukiukwaji wa Katiba na sheria,” alisema.

Alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba alikiri kwamba tume haikuwa katika nafasi ya kuwapatia walalamikaji Fomu 34A, siku tatu baada ya matokeo kutangazwa na akasisitiza kwamba walikuwa wanazingatia Fomu 34B ambazo ziliwasilishwa zote. Hiyo nayo ilisababisha maswali.

Alisema, “Wajibu wa IEBC hni kuhakikisha mfumo wa upigaji kura ni rahisi, wa uhakika, salama na unaowajibika. Namba lazima zioane. Wakenya walisimama katika mistari mirefu kwa saa nyingi na kupiga kura kisha baada ya hapo mfumo ukawa haupenyeki. Hatuwezi kuthibitisha kwamba Uhuru Kenyatta alipata kura nyingi.”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here