SHARE

Rais Robert Mugabe ametinga jijini New York nchini Marekani katika staili ya aina yake, msafara wake ukiwa umejaa watu wasiohusika katika kazi za rais.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 sasa ameongozana na msafara wenye watu 70, miongoni mwao ni wanawe na mjukuu wake.

Wanawe hao ni Bellarmine Chatunga, Bona na Simbanashe. Wapo katika msafara huo huko New York kwa gharama za walipa kodi wa Zimbabwe.

Zaidi ya hapo, wiki iliyopita vile vile kulienea taarifa kwamba kijana mwingine wa mke wa Mugabe, Grace, anayeitwa Russel Goreraza naye atapachikwa kwenye msafara huo.

Inaelezwa kwamba ingawa mkutano anaokwenda kushiriki Rais Mugabe ulipangwa kuanza Septemba 19 hadi 23 wiki hii, lakini msafara huo uliondoka jijini Harare, Zimbabwe mapema zaidi, yaani siku tatu mapema zaidi.

Taarifa za awali zilibainisha kwamba kila aliyekuwamo kwenye msafara huo atalipwa posho ya kujikimu ya dola za Marekani 1,500 kila siku. Taarifa hizo zinatanabaisha zaidi kwamba msafara huo kwa ujumla wake utagharimu dola za Marekani milioni moja.

Kwa miaka kadhaa sasa, Mugabe amekuwa akihudhuria mkutano huo mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN-General Assembly) lakini wakosoaji wake wamekuwa wakieleza ya kuwa, uhudhuriaji wake huo hauna tija kwa kuwa hana jambo lolote la mafanikio linalomwezesha kujivunia mbele ya viongozi wenzake wakuu wa nchi mbalimbali duniani.

Lakini Mugabe kwa upande wake amekuwa akitumia jukwaa hilo kueleza kutoridhishwa kwake na hatua ya jumuiya ya kimataifa kuitenga nchi yake, na amekuwa akitumia lugha ‘kali’ kuwasilisha ujumbe wake huo, lugha zinazowakwaza viongozi wa nchi za Magharibi.

Ingawa msafara wa Mugabe unatumia mamilioni ya fedha lakini hiyo haina maana kwamba hali ya kifedha kwa upande wa serikali yake ni nzuri. Ni kwamba hivi karibuni tu serikali hiyo imesimamisha mchakato wa kuchapisha hati za kusafiria kwa kushindwa kuingiza nchini humo karatasi kwa ajili ya kazi hiyo.

Hali ya uchumi Zimbabwe imegusa hadi uendeshaji wa kampuni kadhaa nchini humo ambazo baadhi zimekwishafungwa na wafanyakazi kupoteza ajira, sababu kuu ikitajwa ni uhaba wa mzunguko wa fedha.

Lakini kwake Mugabe kipaumbele ni safari zake na mara kwa mara amekuwa akisafiri kuelekea nchini Singapore kwa ajili ya matibabu.

Kuhusu safari yake hiyo ya Marekani yenye msafara wa watu 70, mmoja wa wanadiplomasia ameeleza kwamba Marekani ilihoji si tu kuhusu ukubwa wa msafara bali hata aina ya wahusika.

“Hati zao za kusafiria ziliwasilishwa katika ubalozi wa Marekani wiki iliyopita kwa ajili ya mchakato wa kupatiwa viza (visa), lakini maofisa wanaohusika walihoji kuhusu idadi ya wanaosafiri na walikataa kutoa viza kwa mmoja wa wanahabari kutoka chombo cha habari cha serikali,” kinaeleza chanzo kimoja cha habari kutoka duru za kidiplomasia kuhusu safari hiyo ya Mugabe inayotajwa kudumu kwa siku 10 hivi.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here