SHARE

ZAIDI ya watu 2,000 wamejitokeza kuwania nafasi 45 za ajira za watendaji wa kijiji wilayani Kibiti zilizotangazwa na halmashauri hiyo mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Alvera Ndabagoye, aliiambia gazeti la Nipashe jana kuwa baada ya kutoa tangazo hilo, walipokea zaidi ya maombi 2,000 ambayo kwa sasa wanaendelea kuyafanyia uchambuzi.

Halmashauri hiyo ilitangaza nafasi za ajira za watendaji wa kijiji ambao watakwenda kuziba mapengo ya waliofariki dunia na waliokuwa na elimu ya darasa la saba.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, mwisho wa kutuma maombi hayo ilikuwa Septemba 11.

Kibiti ni miongoni mwa wilaya tatu za mkoa wa Pwani zilizokumbwa na mauaji ya viongozi wa ngazi mbalimbali yaliyotekelezwa na watu wasiofahamika tangu mwaka juzi.

Kutokana na kushamiri kwa mauaji hayo na vitisho vilivyokuwa vikitolewa na wauaji dhidi ya viongozi, baadhi ya watendaji wa vijiji waliamua kukimbia makazi yao wakihofia kuuawa.

Hali ya kurejesha amani wilayani humo ilitokana na juhudi za Jeshi la Polisi nchini chini ya mkuu wake, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, ambaye baada ya kuteuliwa alifanikiwa kukomesha mauaji hayo na polisi ilitangaza kuwaua watuhumiwa wa mauaji 13 ambao walikuwa wakitekeleza mauaji katika wilaya za Mkuranga, Rufiji na Kibiti yenyewe.

MATUKIO YA MAUAJI
Tangu mwaka jana, kumekuwa na matukio ya aina hiyo mkoani humo. Zaidi ya viongozi 26 wakiwamo watendaji na polisi waliuawa huku polisi wakiwaua watuhumiwa saba.

Mei, mwaka jana, matukio matatu yalitokea ambayo ni kuuawa kwa kupigwa risasi mwenyekiti wa kijiji cha Nyambunga, Saidi Mbwana.

Aidha, Oktoba aliuawa Ofisa Mtendani wa Kijiji cha Nyambuga, Ally Milandu, baada ya kuvamiwa na watu wanne waliomshambulia kwa kumpiga risasi na mwezi uliofuata, wenyeviti wawili wa vitongoji vya kijiji cha Nyambunda waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, mwaka huu, katika kijiji cha Nyambunga kitongoji cha Mkwandara aliuawa mfanyabiashara Oswald Mrope kwa kupigwa risasi mbele ya familia yake.

Februari pia yalitokea matukio mawili. Katika tukio la kwanza, majambazi walivamia nyumba ya mwenyekiti wa kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga, ambaye alifanikiwa kutoroka, lakini wahalifu hao walirejea na kuimwagia mafuta nyumba yake na kuichoma moto.

Tukio la pili katika mwezi huo ni lile la mauaji ya Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kibiti (OC-CID), Peter Kubezya, na Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji Mapato ya Ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na mlinzi Rashid Mgamba ambao aliuawa kwa kupigwa risasi.

Mwezi Machi, Jeshi la Polisi liliwaua watu watatu katika Daraja la Mkapa walipojaribu kukwepa vizuizi vitatu vya barabara wakiwa na pikipiki.

Aprili, mwaka huu, askari wanane waliokuwa kwenye gari la polisi wakitoka kubadilishana lindo na wenzao walipofika eneo la Mkengeni, Kata ya Mjawa wilaya ya Kibiti, walishambuliwa majambazi na kuuawa kwa risasi.

Katika tukio hilo askari mmoja alijeruhiwa, lakini baada ya tukio hilo Jeshi la Polisi liliwaua watu wanane waliodaiwa kuwa majambazi baada ya kubaini maficho ya muda ya majambazi hao na katika majibizano ya risasi, polisi waliwaua wanne.

Nao viongozi wawili ambao ni kada wa CCM Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani, Amir Chanjale na aliyekuwa Katibu wa chama hicho, Kata ya Bungu wilayani Kibiti, Arife Mtulia, waliuawa Mei, mwaka huu, kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here