SHARE

Vyombo vya habari nchini Uganda vimezuiwa kuonyesha moja kwa moja matangazo ya Bunge ambalo linaendelea na vikao.

Mkurugenzi wa Tume ya Utangazaji nchini humo, Godfrey Mutabuzi amesema redio na runinga zote haziruhusiwi kurusha matangazo ya Bunge moja kwa moja kuanzia jana Alhamisi.

Amesema sababu ya Bunge kutoonyeshwa moja kwa moja ni za kiusalama.

Wabunge nchini Uganda walipigana juzi Jumatano ndani ya ukumbi wa Bunge wakiwa katika siku ya pili ya kikao cha kujadili muswada wa kuondoa ukomo wa miaka ya kugombea nafasi ya Urais kwa mujibu wa Katiba ya Taifa hilo.

Katika ugomvi huo, wabunge walirushiana viti na kuharibu vipaza sauti. Kikao hicho kiliongozwa na Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga.

Ugomvi huo ulianza pale Spika alipochukua hatua ya kuwafukuza wabunge wapatao 25, wengi wao wakiwa ni wa upinzani kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Mwingine aliyetolewa ndani ya ukumbi ni waziri wa Serikali aliyeshtakiwa kwa kufyatua risasi bungeni Jumanne.

Wabunge wanadai kama kikomo cha umri wa miaka 75 kitaondolewa, basi Rais aliye madarakani sasa atapata mwanya wa kugombea tena mwaka 2021.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here