SHARE

Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Hashim Mgandilwa, Leo tarehe 3/10/2017 amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa mtaa wa Gomvu kata ya Somangila.

DC Mgandilwa aliyeambatana na Mbunge wa Kigamboni Mhe Dkt Faustine Ndungulile, wataalam wa ardhi kutoka wizarani na manispaa ya Kigamboni, walienda kukutana na wananchi hao ikiwa ni katika juhudi za kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mwekezaji (Avic town).

DC Mgandilwa amesema kuwa wapo wananchi hao wamekuwa wakimfuata ofisini wakiwa na madai mbalimbali ikiwemo kutolipwa fidia kabisa, kulipwa pesa kidogo, mwekezaji kujiongezea eneo lililokuwa linasemekana ni buffer zone na halilipwi fidia.

Pia amesema kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na wananchi hao amefanya uchunguzi wa kina juu ya mgogoro huo na sasa anataka kuona kila mwenye haki anapata haki yake.

DC Mgandilwa amewataka wananchi ambao hawakupewa viwanja kama fidia baada ya kuhama katika eneo la uwekezaji wafike ofisini kwake Alhamisi asbuhi na mwekezaji aje na ramani za viwanja vya fidia ili wananchi hao wagawiwe kisha waende kwenye maeneo husika ili kila mtu aonyeshwe kiwanja chake.

“Alhamisi tukutane ofisini na mwekezaji aje na ramani ya viwanja anavyodai vipo tayari Kila mtu agawiwe kisha tuongozane kila mtu akaonyeshwe eneo lake, Nataka mgogoro huu uishe, wananchi wakae kwa amani wafanye kazi” Alisema Mgandilwa na kuongeza kuwa haitambui buffer zone, ni eneo halali la wananchi.

Aidha ameongeza kuwa baada ya hatua ya kwanza ya kugawiwa viwanja ndipo wataanza zoezi la pili la kushughulikia ambao waliopata pesa kidogo na ambao hawakulipwa kabisa.

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Kigamboni Faustine Ndugulile amesema kuwa wananchi waendelee kuwa na subira na kuwa serikali itahakikisha haki inatendeka na kuwa nayeye yuko pamoja nao mpaka hatua ya mwisho

Dkt Ndungulile amewasema kuwa kama kuna watu walifanya ujanja na kuwadhulumu wananchi hao haki yao, wafanye haraka ili wananchi hao wapatiwe wanachostahili kwani wamehangaika kwa muda mrefu sasa.

Baada ya Mkutano huo DC Mgandilwa aliwaongoza wananchi wa Kigamboni katika upimaji wa mipaka ya eneo hilo ili kujua kama wananchi wameingia kwenye buffer zone au muwekezaji ndiyo ameingia.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni Rahel Muhando amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inapenda wawekezaji lakini lazima wafuate sheria na taratibu za nchi ili kila upande ufaidike.

Mradi wa AVIC TOWN umechukua ekari 710 na kumekuwepo kwa mgogoro wa ardhi kwa muda wa miaka 8 kati muwekezaji AVIC na wananchi ambao wanadai haki zao kudhulumiwa, ambapo muwakilishi wamuwekezaji huyo Joseph Chagama amesema wameishalipa fidia yote ya zaidi ya bilioni 1 kwa Wizara ya Fedha kupitia akaunti ya Wizara ya Ardhi ambapo watu 72 ndiyo watalipwa huku baadhi wakiwa wamelipwa lakini wengine bado hawajalipwa kwa kutofuata utaratibu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here