SHARE

KIONGOZI wa upinzani hapa Kenya, Raila Odinga, amejitoa katika uchaguzi wa marudio wa baadaye mwezi huu.

Odinga alisema kujitoa kwake kutaipa tume ya uchaguzi muda wa kutosha kuingiza marekebisho ambayo yatasaidia kupatikana kwa uchaguzi halali zaidi.

Mahakama ya Rufani ilifuta matokeo ya kura ya awali iliyopigwa Agosti 8 baada ya kugundua kasoro kadhaa na kuutangaza kuwa “si wa wazi au unaoeweza kuthibitishwa”.

Tume ya uchaguzi ilikuwa imemtangaza rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta kuwa mshindi.
Ilisema Kenyatta alishinda kwa tofauti ya kura milioni 1.4.

Uchaguzi wa marudio ulikuwa ufanyike Oktoba 26, lakini Odinga alisema jana: “Tumefikia hitimisho kuwa hakuna nia kwa upande wa IEBC (tume ya uchaguzi) kufanya mabadiliko yoyote katika maandalizi yake na watumishi… Dalili zote zinaonyesha uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa wa ovyo kuliko uliopita.”

Kwa sababu hiyo, alisema, “ukizingatia maslahi ya watu wa Kenya, eneo (la Afrika Mashariki) na dunia kwa ujumla” ni busara kujitoa kwenye kinyang’anyiro.

Chama hicho cha upinzani kilishasema kwamba kushiriki kwake katika uchaguzi kulitegemea kufanyika kwa marekebisho.

Kinaamini uchaguzi utalazimika kufutwa kutokana na kujitoa kwa Odinga, kuruhusu “muda wa kutosha wa kufanya marekebisho muhimu kwa ajili ya kuendesha uchaguzi ambao unaendana na misingi ya katiba, sheria husika na katiba”.
Serikali iliwahi kusema kuwa uchaguzi huo utafanyika kama kawaida na rais kuapishwa.

Odinga pia ameitisha maandamano leo, akitumia kauli mbiu “bila marekebisho, hakuna uchaguzi”.

Mwezi uliopita, mkurugenzi wa mashtaka wa Kenya, Keriako Tobiko, aliomba polisi na taasisi ya kupambana na rushwa kuchunguza kama maofisa wa tume ya uchaguzi walifanya makosa yoyote ya kiuchaguzi ama kijinai.

Aliwataka wapelelezi kuchunguza madai kuwa maofisa wawili wa ngazi ya juu wa upinzani waliingilia kwa jinai mfumo wa utunzaji kumbukumbu wa kompyuta wa tume.

Ingawa hakuna mtu ambaye amelaumiwa, alisema zaidi, hilo halizuii korti kuagiza uchunguzi.

BBC


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here