SHARE

Presha kubwa ilikuwa juu ya Argentina na kocha wao, lakini presha mara dufu ilikuwa mabegani mwa Lionel Messi katika kampeni zao kufuzu Kombe la Dunia 2018.

Wengi walishakata tamaa na wengi waliamini Messi ana nafasi ndogo kushiriki kombe la dunia mwakani lakini alichofanya alfajiri ya leo kinathibitisha kwamba yeye ni Simba kama jina lake Leo.

Lionel Messi amewabeba Argentina mabegani mwake na kuwapeleka kombe la dunia baada ya kufunga mara tatu katika ushindi wa bao 3 kwa 1 dhidi ya Ecuador.

Mabao ya Messi yamemuweka kwenye vitabu vya rekodi vya Conimobel ambapo anakuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 21 wakati wa michezo ya kufuzu kwenye ukanda huo.

Ushindi wa Argentina umetokana na sare ya Colombia dhidi ya Peru ambao wamefungana goli moja moja na kuwafanya Argentina kumaliza nafasi ya 3, James Rodriguez aliifungia Colombia kabla ya Paulo Guererro kusawazisha.

James Rodriguez Colombia

Chile ambao hadi jana walikuwa nafasi nzuri walipigwa bao 3 kwa 0 na Brazil na kupelekwa hadi nafasi ya 6 itakayowalazimu kukosa kombe la dunia, mabao ya Brazil yakifungwa na Paulinho na Gabriel Jesus (2).

Alexis Sanchez, Chile

Uruguay wamekaa katika nafasi ya pili baada ya kuikung’uta Bolivia 4 kwa 2 Luis Suarez akifumania nyavu mara mbili, Cavanni na Martin Caceres moja kila mmoja.

Kwa matokeo haya sasa timu za taifa za Brazil, Uruguay, Argentina na Colombia zimefuzu moja kwa moja kombe la dunia mwakani huku Peru watalazimika kucheza kwanza mechi za mtoano.

Concacaf nako ndoto za USA kushiriki fainali za kombe la dunia zilizimwa baada ya Trinidad and Tobago kuwapiga goli mbili kutoka kwa Alvin Jones na la kujifunga la Omar Gonzalez huku bao la USA likifungwa na Christian Pulisic.

Christian Pulisic USA Trinidad

Vinara wa kundi Mexico walipigwa bao 3 kwa 2 na Honduras lakini haikuwatoa kileleni huku Honduras wenyewe wakimaliza nafasi ya nne itakayowalazimu kucheza mtoano dhidi ya Australia.

Panama waliifunga Costa Rica bao 2 kwa 1 kupitia kwa Gabriel Torres na Roman Torres huku bao la Costa Rica likiwekwa kimiani na Johan Venegas lakini timu zote hizo zina tiketi ya kombe la dunia.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here