SHARE

Watanzania wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu, misingi na vitendo katika kuienzi kazi kubwa ya uzalendo ambayo ameifanya katika nchi yetu.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mh. Ali Hapi alipoongoza kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya pamoja na Jeshi kwa kufanya usafi wa Mazingira kwenye eneo alilokuwa akiishi Baba wa Taifa.

Amesema Usafi huu ni kumuenzi na pia ni katika kukumbuka mchango mkubwa ambao Muasisi wetu Baba wa Taifa aliufanya katika nchi yetu.

“Kwanza tumeamua pamoja na kamati ya ulinzi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwenye Wilaya yetu kumuenzi baba wa Taifa kuelekea tarehe 14 October kwa kufanya usafi kwenye Mazingira ambayo Baba wa Taifa alikuwa akiishi na sasa Mama yetu, Mama Maria Nyerere anaishi. “Amesema Hapi

Ameongeza kuwa usafi huu ni sehemu ndogo sana ya kuenzi yale mema mengi ambayo Mwl Nyerere aliyafanya ikiwemo misingi aliyotuwekea Kama Taifa, ya uzalendo, uadilifu, umoja, amani na mshikamano .

“Tunatoa wito kwa wananchi wote wa Kinondoni kujitolea kumuenzi Mwalimu kwa vitendo kwa kufanya kazi, kusafisha maeneo yao, na kuhakikisha kwamba wanawafundisha watoto wao na vizazi vinavyokuja uzalendo wa kuipenda nchi na kuitanguliza nchi mbele, na hilo ndo jambo ambalo Rais wetu mpendwa amekuwa akilihubiri kila siku ‘Amesisitiza Hapi.

Naye Mama Maria Nyerere ameishukuru Serikali kwa mchango wao mzima waliouonyesha kwa kutumia muda wao katika swala la usafi wa Mazingira, pamoja na nyenzo walizonazo katika kumuenzi Baba wa Taifa kwa kufanya usafi kwenye eneo Lake.

Katika hatua nyingine Hapi amewataka watanzania kujiwekea misingi ya kufanya usafi kwenye maeneo yao, na kutambua kuwa usafi wa Mazingira ni sehemu ya Usalama wa nchi.

Imetolewa na
Kitengo cha Uhusiano
Manispaa ya Kinondoni.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here