SHARE

Kwa mara nyingine tena serikali ya Misri imeongeza muda wa sheria ya hali ya hatari nchini humo kwa miezi mitatu mingine.

Dikrii ya kuongeza muda huo imechapishwa katika gazeti rasmi la serikali leo Alkhamisi, na agizo hilo litaanza kutekelezwa upya kuanzia kesho Ijumaa.

Misri imekuwa chini ya sheria ya hatari inayoongezwa muda baada ya kila miezi mitatu tangu Disemba mwaka jana, kufuatia wimbi la mashambulizi ya kigaidi dhidi ya makanisa, ambapo watu wasiopungua 100 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Mwezi Aprili mwaka huu serikali ya Misri ilitangaza sheria ya hali ya hatari nchini humo baada ya shambulio jingine la kigaidi lililotekelezwa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ambalo lilipelekea watu 45 kuuawa.

Kwa mujibu wa sheria hiyo ya hali ya hatari, vikosi vya usalama vina mamlaka ya kumtia mbaroni mtu yeyote na wakati wowote.

Kukandamizwa maandamano ya wapinzani MisriĀ 

Hayo yanajiri huku jumuiya mbalimbali za kutetea haki za binadamu zikiendelea kulalamikia kile zinachokitaja kuwa ukandamizaji na kukithiri kutolewa hukumu za vifo dhidi ya raia katika nchi hiyo.

Misri imekuwa ikikabiliwa na machafuko, mauaji, maandamano na mashambulizi katika pembe mbali mbali za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hasa baada ya tarehe 3 Julai, 2013 wakati jeshi la nchi hiyo lilipofanya mapinduzi ya kijeshi na kumuondoa madarakani Mohammad Morsi, rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kidemokrasia.

 


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here