SHARE

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu amesema kwamba matukio yanayoendelea hayawezi kuwaziba midomo au kusimamisha kazi zao bali yanazidi kuwaimarisha zaidi kisiasa.

Leo wakizungumza kwenye makao makuu ya Chama jijini Dar es salaam mbele ya wanahabari, Mwalimu amekanusha tetesi za kwamba chama kimefungwa mdomo na kubweteka tangu tukio la kushambuliwa kwa Mwanasheria wao Mkuu wa chama na Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Mwalimu amesema kwamba tukio la kushambuliwa kwa kiongozi wao hakujafanya chama hicho kushindwa kuendelea na shughuli za chama na badala yake wanaendelea kuimarisha chama kupitia kampeni ya Chadema ni Msingi zinazoendeshwa nchi nzima pamoja na kuweka mikakati ya kushinda kwenye uchaguzi mdogo.
“Tupo kwenye vikao vizito vya kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye uchaguzi mdogo uliotangazwa. Tukio hili la Lissu halijafanya shughuli za chama zisimame, Shughuli zinaendelea kama kawaida. Mikoani na makao makuu ya chama mambo yetu yanaenda kama awali. Tuna kampeni kubwa inaendelea nchi nzima inaitwa ‘Chadema ni msingi’. Hatuwezi kusimama na kwanini tusimame tunazidi kuimarika kila siku. Kwa yanayoendelea wapo wanaodhani yatatuziba midomo lakini ndo yanatupa hamasa zaidi ya kuendelea kuwatetea” Mwalimu.
Ameongeza kwamba “Napenda kuwahakikishia Watanzania hatujatetereka kwa yanayoendelea tupo imara, chama hiki ni chao kitaendelea kuwa kipaza sauti zao”.
Aidha Mwalimu amesema kuhusu afya ya Mh. Lissu siku chache zijazo watatoa taarifa kuhusu maendeleo yake.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here