SHARE

MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amesema madai ya yeye kuhusishwa na tuhuma za kuchoma shule moto hayana ukweli wowote.

Alisema madai hayo ni ya uzushi, umbea, unafiki na majungu dhidi yake.

Amesema pamoja na tuhuma hizo kuwa ni nzito, lakini amezipuuza na kuwa atashangaa iwapo Jeshi la Polisi halitachukua hatua dhidi ya tuhuma hizo, ikiwa ni pamoja na kuwahoji na kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wote watakaobainika.

Gambo aliyasema hayo jana ofisini kwake, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya sekta mbalimbali katika Mkoa wa Arusha.

Alisema kuwa, polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, hawafanyi kazi kwa mashinikizo, hiyo tuhuma ipo na polisi wawe huru kulifanyia kazi jambo hili, wachukue maelezo ya wahusika na wapeleke suala hilo mahakamani.

Alisema kuwa, wapinzani katika Mkoa wa Arusha wameshindwa kusoma ramani, wameshapotezana na kuwa kila siku wamekuwa wakitunga vituko na vioja, ikiwa ni pamoja na kuchokoza viongozi ili wakamatwe na waonekane wanaonewa.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema aliamua kuwapuuza, ila amefarijika kwa sababu madiwani na wabunge wa upinzani katika mkoa huu wameacha kazi ya maendeleo kwake, wakuu wa wilaya na wakurugenzi.

LEMA, NASSARI

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo aliwarushia kijembe Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki, kwa kudai wabunge hao wamekuwa wakitembea na flash wanayodai ina ushahidi wa namna baadhi ya madiwani wao walivyonunuliwa, badala ya kuhangaika na matatizo ya wananchi.

Alisema kuwa, hivi sasa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri ndio wamekuwa wabunge na yeye amekuwa mwenyekiti wa wabunge kutokana na wabunge wa majimbo hayo kutokuwapo.

KUNUNULIWA MADIWANI

Akizungumzia madai ya kununuliwa kwa madiwani waliohama Chadema na kuhamia CCM, alisema kuwa si kweli, bali madiwani hao walihama kwa sababu wamekunwa na utendaji wa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema wanasiasa kuhama vyao ni kitu cha kawaida na kudai kuwa, madiwani wengi waliogombea nafasi hizo kupitia Chadema, zamani walikuwa madiwani wa CCM na kuuliza waliwapa kiasi gani cha fedha kwa madiwani hao wakahama.

Alidai kuwa, alishawahi kuwashauri upinzani na kuwaambia wasipobadili aina ya siasa kwenye serikali hii ya awamu ya tano ambayo imejielekeza kuhangaika na shida za wananchi, wakajiingiza kwenye porojo na usanii wao, watapotea.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here