SHARE

Fedha ndiyo kila kitu. Wapo wengi wanaoamini katika msemo huu ingawa wengine wanamtazamo tofauti japokuwa ukweli unabaki pale pale kuwa, fedha ina uwezo wa kufanya mambo mengi na makubwa.

Kampuni kubwa ya kutengeneza ndege ya Boeing ya chini Marekani, imetengeneza ndege binafsi ya kifahari zaidi kuwahi kutengenezwa duniani, ndiyo!

Ndege hiyo aina ya Boeing 747-8 VIP inaelezwa kuwa ndiyo ya kifahari zaidi duniani na muundo wake wa ndani ni kama hoteli ya kifahari. Unaposafiri na ndege hiyo ni kama vile hausafiri bali upo ndani ya hoteli ya kifahari inayopaa angani.

Kampuni ya Boeing ilitengeneza ndege hiyo ya aina yake kwa oda maalumu na walichokifanya ni kusaidiana na washirika wake kubadilisha muundo wa ndani wa iliyokuwa kubwa ya abiria aina ya Boeing 747-8 kuwa ndege binafsi ambayo iligharimu Dola za Marekani milioni 380 sawa na Sh bilioni 700 na milioni 266 za Kitanzania.

Kwa kipindi kirefu Boeing walikuwa wakificha mmiliki wa ndege hiyo hadi ulipofika wakati wa kuikabidhi na kugundulika kuwa ni ya familia ya kifalme ya Qatar, nchi ambayo ni tajiri kuliko zote duniani.

Ndege aina ya Boeing 787-8 ya abiria yenye uwezo wa kubeba abiria 450 ndiyo ambayo kampuni ya Greenpoint Technologies ya Marekani ilibadilisha muundo wake wa ndani na kutengeneza ndege binafsi ambayo ni kama kasri kwa ndani kwa ajili ya matumizi binafsi ya familia ya kifalme.

Greenpoint Technologies ni kampuni maarufu nchini Marekani kwa utengenezaji wa muonekanano wa ndani wa ndege binafsi pamoja na ndege za wakuu wa nchi kupitia kampuni ya Boeing.

Utengenezaji wa ndege hiyo umekuwa gumzo kubwa na suala la nani alikuwa mmiliki wake ilikuwa ni siri kubwa. Ndege hiyo inagharimu mara tatu ya ndege binafsi ya kifahari ya milionea na mfanyabiashara ambaye kwa sasa ni Rais wa Marekani Donald Trump. Utengenezaji wa ndani ulifanyika Marekani na kumaliziwa nchini Ujerumani.

Ndege hiyo kwa ndani ni kama upo kwenye jumba la kifahari. Kuna makabati ya kuwekea vitu mbalimbali, kuta zenye picha, silingi bodi. Pia ndege hiyo ina sebule kubwa na ya kifahari, sehemu ya kulia chakula (dining room), ofisi pamoja na vyumba vya kulala.

Ndege hiyo ya aina yake, inaelezewa kuwa ndiyo ya kwanza kutengenezwa kwa namna ya pekee huku mabilioni ya dola yakitumika tangu wazo la kuwa na ndege ya kifahari zaidi duniani kuijia familia ya kifalme. Kabla ya kuanza kutengenezwa, mmiliki alikutana na wataalamu mbalimbali ambao walionekana wangekuwa na uwezo wa kutengeneza mwonekano wa ndani. Baadhi ya kampuni hayo ni pamoja na BMW, Design works USA na Giugiaro Design kabla ya kuamua kuichagua kampuni ya Greenpoint Technologies kufanya kazi hiyo.

Marekani pamoja na kuwa na matajiri wakubwa kama kina Bill gates, Warren Buffet na wengineo, bado hakuna tajiri aliyeweza kuvunja rekodi kwa kuwa na ndege ya kifahari kama hiyo.

Pamoja na ukubwa wake, ndege hiyo inaelezewa kuwa ni ya mwendo kasi kuliko kawaida huku ikiwa na uwezo wa kubeba watu 100. Wataalamu wanasema, kwa kutumia ndege hiyo, mtu anaweza kuwa London nchini Uingereza jioni na kuondoka kwenda kufanya starehe kama kwenda Club katika jiji la New York nchini Marekani. Wakati wa kurudi, ndege hiyo haitahitaji kuongeza mafuta kwa ajili ya safari ndefu ya kuvuka bahari ya Atlantic kama ambavyo ndege nyingine zingehitaji.

Uwezo wa kutua kwenye viwanja tofauti tofauti pamoja na kutumia vifaa vya kawaida vinavyosaidia ndege kutua ni kati ya sifa zinazofanya ndege hiyo kuwa ya kipekee.

Naam, familia ya kifalme ya nchi tajiri zaidi duniani ya Qatar ndiyo wamiliki wa ndege hii.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here