SHARE

Pamoja na kuumizwa sana na kauli ile nilijitahidi kuvumilia kwakuwa nilikuwa najua fika hali ya kutokuwa mvumilivu ingenirudisha nyuma kama ambavyo imetokea mara kadhaa ninapokuwa na bwana Mnaro. Safari hii nikafanikiwa na kushusha kabisa hasira nilizokuwa nazo na kuonesha utulivu ambao najua hata Mnaro mwenyewe hakuutegemea.

“Tunafanyaje sasa? Nadhani muda wa kwenda Muifufu umefikia, hatupaswi kumuacha huyo Magugi aendelee kufanya atakacho, ni bora kumuwahi mapema kwamaana kadri muda uendavyo na yeye anajipanga” nilianzisha upya maongezi ili kumshawishi bwana yule nikijaribu kuonesha utulivu wa hali ya juu ili nisionekane mwenye kukurupuka.

“Ni muda muafaka wa kwenda Muifufu sikatai, ila jambo la msingi zaidi ni wewe kujifunza mbinu ambazo zitakuwezesha kuwa salama ndani ya Muifufu, kama ambavyo nilikueleza awali itakubidi kuwa mchawi, na sasa niko tayari kuanza kukufundisha mbinu hizo” aliweka kituo akanitizama nami nikauliza kwa shauku “ni lini tutaanza sasa mafunzo hayo” naye akanijibu “muda wowote ukiwa tayari, hata leo kama ukitaka” nikajikuta nimeingiwa na faraja moyoni mwangu na matumaini ya kumpata mke wangu yakanijia tena kwa kasi kubwa “Mafunzo haya yatatuchukua muda gani mpaka kuyamaliza?” niliuliza tena ili kujua ni muda kiasi gani ulikuwa umesalia mpaka safari ya Muifufu.

“Hiyo inategemea kasi yako ya kuelewa, siku tatu zinaweza kutosha kama una kasi nzuri, lakini kama huna kasi ya kutosha inaweza kutuchukua miaka” kitu pekee ambacho nilikua nikikitaka kwa wakati ule ni kwenda mahali alipo mke wangu kwa gharama yoyote. Kuingia kwenye mafunzo ya uchawi sikuona kama ni tatizo na nikaamini haitonichukua muda kufuzu mafunzo hayo kwa maana siku zote penye nia pana njia.
“Naomba tuanze leo hayo mafunzo” niliomba na Mnaro akakubali na kunitaka nijiandae kwa jambo hilo usiku wa siku hiyo kisha akaondoka.

Niliendelea kujipumzisha pale kitandani baada ya kuangalia muda na kuona ni saa moja tu toka tuingie kupumzika na kuona haukuwa wakati muafaka wa kuongea na baba yangu juu ya jambo lile baadala yake nilipaswa kumuacha apumzike huku na mimi nikijipatia nafasi ya kupumzika zaidi nikiamini kazi ya usiku wa siku hiyo itakuwa sio ya kitoto, na kweli usingizi ulinichukua kama ambavyo nilitaka.

Nilifumbua macho kutoka kwenye ndoto ambayo nilikuwa nikiota kuwa Mnaro ananiita na kweli nikamkuta akiwa amesimama kando ya kitanda changu pale chumbani.. “amka haraka tuwahi kabla hakujapambazuka, na leo itakuwa mara ya mwisho kukufuata itabidi uwe unakuja mwenyewe mafunzoni” alisema Mnaro ambaye alikuwa amevalia kivazi mfano wa nguo ya ndani ila kilikuwa kimetengenezwa kwa ngozi, alikuwa ni karibu tu na mtu aliye uchi. Nikawa naomba kimoyomoyo mafunzo hayo yasiwe ya uchawi ule wa kutembea uchi ambao huwa nausikia.

Alinipa kitu kama kijiti kidogo mithili ya njiti ya kibiriti akanitaka nikishike kwa kukibana katika kidole changu cha mwisho cha mkono wa kushoto na kisha kuniambia “ukiwa umekibana kijiti hicho namna hiyo unaweza kupenya kupita hapa ukutani na kutokea nnje, unatakiwa tu kuhakikisha mlango umefungwa kwa maana ukiwa wazi hauwezi kupenya, jambo lingine ni imani, unatakiwa kuamnini unachokifaya vinginevyo uchawi huwa unashindwa kukusaidia”

Niligeuka na kuangalia mlango wa chumba changu na kuona ukiwa umefungwa, ikabaki tukio la kupenya kupitia ukutani kutoka nnje ya nyumba! “Basi wacha nimuage baba maana anweza kuamka akanikosa kisha akapatwa na wasiwasi” nilitoa ombi nikianza kuongoza kuuelekea mlango wa chumba changu “hapana, haina haja. Lengo la uondokaji wa aina hii ni kumfanya mtu anayebakia kutojua kama haupo, ataendelea kukuona ukiwa umelala palepale mpaka utakaporudi” alielezea Mnaro maelezo ambayo yalinishangaza sana “vipi kama ataamua kuniamsha sasa? Si nitashindwa kuamka na kumtia wasiwasi uleule?” niliuliza swali lingine ambalo nalo alilijibu “unatakiwa kunuia ambavyo unataka mambo yatokee ukiwa haupo, kwa mfano unaweza kunuia kuwa iwapo mtu ataingia chumbani asikuamshe naye atakuwa mzito kufanya uamuzi wa kukuamsha na kuamua kukuacha ulale” niliyaelewa vizuri maelezo yake lakini nilishangaa kwanini anakwepa sana wazo la kumuaga baba hali ya kuwa hili sio jambo la siri kwake kwamaana anaijua mipango inayoendelea “kwani kuna ubaya wowote kama nikimuaga?” niliamua kuuliza baada ya kushindwa kujipatia mwenyewe najibu ya maswali yangu.. “wachawi huwa hawaagi wanapotoka kwaajili ya kwenda kwenye shughuli za kichawi, mafanikio huwa sio makubwa kwenye safari kama mchawi ataaga” nilimuelewa na kuamua kufanya kama ambavyo likuwa akiniagiza.

“kibane vizuri hicho kijiti kisha upite hapo utokee nnje” alinielezea Mnaro akinioneshea kwenye ukuta wa chumba kile, nami nikatembea polepole kuelekea kwenye ukuta ule nikiuvaa polepole kuona kama utaniruhusu kupita baadala yake nilijikuta nikijigonga ukutani, sikufanikiwa kupenya. Nikageuka na kutizama Mnaro ambaye alikuwa akitikisa kichwa kusikitika “nimekwambia mambo mawili ambayo ni lazima yatimie ili uweze kupenya.

itaendelea sehemu ya 12


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here