SHARE

nilibaki pale ndani nikifikiria mengi na katikati ya mawazo nikakumbuka adhma kuu ya kuwepo Muifufu, mke wangu kipenzi!.. sijui atakuwa wapi Samia wangu!, niliwaza na kujikuta nikitembea kutoka nnje ya eneo lile bila ya kujua nilikuwa nakwenda wapi, nikajikuta nafuata njia ileile ambayo ilinileta katika nyumba ile nikimfuatilia Sauda, nadhani ni kutokana na kutopajua pengine popote!..

nilifika mpaka kwenye uwanja ambao tulikuwepo masaa machache yaliyopita lakini kitu cha ajabu ni kuwa lile jumba la kifahari ambalo ndio makazi ya Magugi halikuwepo tena pale ambapo lilikuwepo mwanzo! uwanja ulikuwa mtupu, nilistaajabishwa kwa muda mfupi juu ya kutokuwepo kwa jumba lile, nikafikia kudhani kuwa pengine nilikuja eneo tofauti lakini nikajiridhisha kuwa sikuwa nimepotea, ni penyewe haswa ila uchawi ulikuwa umefanyika tayari bila shaka ni uchawi wa aina ileile ambao uliuficha mji wa Muifufu ukakosa kuonekana duniani ikiwa upo humohumo!.. Nikaamua kuwa ni bora nirudi tu kwenye yale makazi yangu ya muda kuliko kuwepo kwenye mazingira yale yasiyoeleweka na mwisho wake kunasa mikononi mwa Magugi kirahisi!…

muda huu kagiza kalikuwa kameanza kuingia, hali ya Muifufu ilikuwa ni tulivu mno, hakukuwa na watu wengi kama iwavyo dunia ya kawaida hasa mida hii ya jioni kila mtu akirudi nyumbani kutoka kwenye shughuli mbalimbali!…

nilipokaribia nyumba ile ambayo ndipo nilipokuwa nimewekewa makazi ya muda niliona kundi kubwa la watu wakiwa wamekusanyika pale! lilikuwa ni kundi kubwa kama ambalo lilikuwepo pale kwa Magugi wakati wakinitafuta!. Nikasogea kwa taadhari sana na kugundua kuwa nyumba ile ambayo nilifikia ilikuwa ikiwaka moto! kwa mbali pia niliona watu wawili wakiwa wamefungwa kwenye miti ambayo bila shaka ilichimbiwa pale chini kwa shughuli ile kwani haikuwepo mwanzo!..

pembeni ya watu wale kulikuwa na jitu lenye misuli mikubwa mno likimchapa mmoja wa watu wale kwa fimbo za mfululizo kisha lilipumzika na kufanya mzungumzo kwa muda mfupi na baadae likamchapa yule mtu mwingine na kufanyanaye mazungumzo pia! sikuweza kuwatambua watu wale ambao walikuwa kwenye mateso yale makali lakini hisia ziliniambia kuwa alikuwa bwana yule ambaye Sauda aliniacha kwake, bwana Mkude!.. Nikafikiria kwenda kujumuika kwenye kundi lile ili kujiridhisha juu ya watu wale ni akina nani na kujua nini hasa chanzo cha mateso yale kwa watu wale!.

Lakini itakuwaje kama tayari wanaijua sura yangu na kufika kwangu pale ikawa kujikamatisha? je kama watu wale wanateswa ili kuonesha nilipo na hawaoneshi kwakuwa hawajui nilipo kwenda kwangu si itakuwa pona yao na matatizo kwangu?! nilijiuliza na kufikia uamuzi wa kujisogeza kwa taadhari mpaka kwenye kichaka kidogo ambacho kilikuwa karibu zaidi na umati ule!, angalau kutokea pale niliweza kushuhudia na kusikia sauti za juu ya kilichokuwa kinaendelea pale!..

“sogezeni hapa zile kuni” nilisikia akiagiza bwana yule mwenye kutoa adhabu na watu ambao walikuwa wamevaa sare wakakimbia na kusogeza mzigo mkubwa wa kuni miguuni mwa watu wale!..
“sheria za Muifufu ni lazima ziheshimiwe, na yeyote mwenye kujaribu kuzivunja adhabu yake ni kifo, nipe moto” alisema mtu yule kisha akaagiza apewe moto na akapewa ukuni uliokuwa ukiwaka moto mkubwa kiasi cha kutoa mwanga naye akakiangushia kwenye kuni zile ambazo zilianza kushika moto kwa kasi na hatimaya kufanya moto mkubwa ambao ulianza kuwaunguza watu wale ambao niliwagundua kuwa walikuwa wale wenyeji wangu huku umati ule ukishangilia tukio lile!…

kwa upande wangu roho iliniuma sana… niliumia kwakuwa sikuwahi kushuhudia ukatili kama ambao ulitendeka pale, lakini pia niliumia mno kwakuwa niliona waziwazi kuharibika kwa mambo ambayo yalikuwa yamepangwa hapo mwanzo!..

usikose sehemu ya 32


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here