SHARE

Ilipoishia…

“kila kitu kitakuwa sawa wakati unaingia Muifufu wewe kuwa tayari kwa safari” alisema mzee yule na safari ya kurudi Muifufu ikawa tayari, nikaondoka kijijini pale nikisindikizwa na wakazi wa kijiji kile mpaka mlimani kisha wakarudi na kuniacha nikipanda mlima ule…

Endelea..

safari ya kupanda mlima ilikuwa na changamoto kama ile ambayo nilikuwanayo wakati wa kuja mlima Kalingisi ingawa safari hii kidogo kulikuwa na unafuu uliotokana na kuijua safari yenyewe tofauti na safari ya kwanza ambapo sikuwa nikijua nilikuwa nakwenda katika safari ya aina gani!..

ugumu wa safari hii ulinikuta mchana wa kwenye saa sita ambapo nilipatwa na kiu ya hali ya juu lakini sikuwa na maji ya kunywa, nilikuwa nimetokwa na jasho jingi sana nadhani sasa yalihitajika maji mwilini kufidia yaliyopotea, lakini ndo hivyo tena, sikuwa na maji hivyo ikanibidi kupambana kiume na safari ile mpaka majira ya saa kumi za jioni ambapo hali ilikuwa mbaya zaidi nikajikuta nikishindwa hata kunyanyua hatua moja ya ziada, hata macho hayakutaka kufanya kazi yake tena na kizunguzungu kikanitawala. Jambo pekee ambalo nilimudu kulifanya ni kukaa chini polepole lakini kabla sijafika chini kabisa nikashindwa kuutawala mwili wangu na kujikuta nikianguka na kupoteza fahamu…

nilipokuja kuzinduka nilijikuta katika mazingira ambayo niliyatambua, hapa ndipo ambapo wenyeji wangu wa Muifufu waliniachia nikaendelea na safari na wao wakarudi Muifufu wakati waliponisindikiza. Hii ni ndoto au hali halisi? nimewezaje kuvuka shughuli nzito ya kupanda na kushuka kwenye mlima ule nikiwa katika hali ya kutojifahamu? nilijiuliza lakini sikupata majibu na kuamua kuachana na jambo lile kwani akili yangu pia ilikuwa imechoka na haikutaka kufikiria zaidi. Nikapata nguvu na kusimama na kujitahidi kutembea kuelekea Muifufu. Hali ya mwili wangu bado ilikuwa dhaifu lakini kutokana na matumaini mapya niliyoyapata nikamudu vizuri kutembea ingawa haikuwa rahisi.

Sasa nakwenda wapi? sijui pa kumpata Sauda na mfadhili wangu bwana Mkude tayari alikuwa ameteketezwa kwa moto pamoja na mkewe na nyumba yao vile vile, nakwenda kufikia wapi?.. nilijiuliza na kuamua kuwa niende kwenye lile shamba ambalo nilimkuta Sauda akiwa na watu ambao walinisindikiza.
Pengine naweza kuwakuta, ila hata nisipowakuta nijificha hukohuko na kuwasubiri kuliko kunasa mikononi mwa Magugi, niliwaza nikiendelea kujikongoja.

Kwa mbali nililiona shamba likiwa na watu wawili waliovalia sare kama ambazo walivaa wale ambao walinisindikiza, nikazidi kujivuta kuelekea walipo ila kwa taadhari wasije wakaniona kwamaana sikuwa nimejua kama walikuwa salama kwangu ama laa!..
Nilipofika kwenye eneo la kuweza kuwatambua watu wale nikapata amani na kuwafuata moja kwa moja!..
walikuwa vijana wale ambao walinisindikiza wakati naelekea mlima Kalingisi..

Nilipowafikia nikajibwaga chini kama mzigo, sikutaka tena kufanya chochote kutokana na uchovu ulioambatana na njaa na kiu ya muda mrefu, mdomo wangu ulikuwa umekauka sana, hata mate hayakuwepo kinywani.
Mmoja wa vijana wale akasogea mpaka ambapo kulikuwa na vitu vyao, akachukua kibuyu na kujanacho pale nilipo na kuanza kuninywesha maji..

katika maisha yangu yote sikuwahi kuona maji yakiwa matamu namna ile, nilikunywa haraka haraka ndani ya muda mfupi yakawa yameisha ndani ya kibuyu nami nikajiachia na kulala chali pale chini shambani, nilikuwa nimechoka sana.
Vijana wale wakakusanya vitu vyao harakaharaka na kuja kunichukua wakinitaka tuondoke, wakaninyanua, nikasimama kisha wakaniweka katikati yao huku mikondo yangu ikiwa mabegani mwao kunirahisishia kutembea. Ama kweli maji ni uhai, nilikuwa na nafuu kubwa kiasi cha kuwataka mabwana wale waniache nitembee mwenyewe, jambo ambalo walikubali nami nikalifanya na kufanikiwa. Tukaenda tukizama zaidi kwenye mashamba na hatimaye tukakutana na kajumba kadogo katikati ya shamba la mahindi..

tukaingia ndani ya nyumba ile, nikaenda moja kwa moja na kujilaza kwenye kitanda ambacho kilikuwemo kwenye Kijumba kile na kupitiwa na usingizi…
Baada ya muda mfupi niliamshwa na vijana wale, walikuwa wameandaa chakula, tukala pamoja ingawa mimi nilionekana kula zaidi kuliko wenzangu ambao walimaliza mapema na kuniacha nikiendelea kula harakaharaka kama mtu ambaye sikuwahi kuona chakula kabla mpaka ambapo nilishiba na kuamua kupumzika huku nikiwataka vijana wale kumfikishia Sauda taarifa za kwamba mimi nilikuwa pale, vijana wale wakanitaka kupumzika huku wakiniambia swala lile niwaachie wao. Nikaendelea kupumzika nikiwaacha wao wakiendelea na mambo mengine..

USKOSE SEHEMU YA 39


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here