SHARE

Baada ya dakika kama tano alikuja mzee ambaye umri wake haukutofautiana sana na Magugi.
“kuna nini cha kuniamshia usikuusiku mabwana?” alisema bwana yule huku akikaa kutusikiliza.
Sikutaka kupoteza muda, nikamuelezea bwana yule juu ya ujio wangu..

“Mnaro alinitaka kukuona wewe ikiwa nitakwama popote, alisema wewe ni tegemezi kubwa kwake” niliongezea uongo kwakuwa mpaka wakati huo nilikuwa nikiamini kuwa mzee yule alikuwa na upendo kwa Mnaro ndio maana hakutoa taarifa kwa Magugi juu ya mwenendo wa Sauda hata baada ya kujua vizuri ambacho Sauda anakipanga kukabiliana na Magugi.
“sasa kijana unataka mimi nikusaidieje?” aliniuliza mzee yule kwa upole kabisa.

“Mimi nataka kujua tu ni namna gani tunaweza kumuokoa Sauda kutoka kwenye kifo ambacho kiko mbele yake” nilijieleza, mzee yule akanitizama kwa utulivu, kisha akaongea “nilimuonya sana Sauda lakini hakutaka kusikia, jambo ambalo mnataka kufanya ni jambo la hatari sana, yani ninyi mmeamua kukitafuta kifo kwa jitihada zote hizo? kijana wangu, amini kuwa Sauda tumempoteza na urudi ukamwambie huyo Mnaro akae hukohuko aliko habari za huku azisahau kabisa kwaajili ya usalama wenu nyote” aliongea mzee yule akionesha waziwazi kutoamini kama Magugi anashindika…

“Mzee wangu mpaka kuwepo hapa nimepoteza vingi sana, siwezi kurudi bila mafanikio ni bora kufa nikitafuta kufanikiwa” nilimjibu mzee yule nikionesha kutokuwa na nia ya kukata tamaa..
“sasa kama ninyi hamuhofii maisha yenu basi niachieni yakwangu, mimi siko tayari kufa hata kidogo” alijibu mzee yule.
Kufikia hapo nikaona kama sina kingine cha kumwambia mzee yule. “wakati mwingine jamii huwataka watu fulani kujitolea kwaajili ya usalama wa wengine wote hata kama kufanya hivyo ni kujiweka mashakani” hatimaye nilipata cha kusema na mzee yule akawa kimya, kama ambaye alikosa cha kusema.
“sawa mzee wangu, sisi tunaondoka ila tunaomba kama huwezi kutusaidia basi angalau usijaribu kutuzuia” niliongea nikisimama kujiandaa kuondoka.. “safari ya mlima kalingisi ilikuwa na mafanikio?”

Aliuliza mzee yule, nikashangaa kuona kuwa alikuwa akijua juu ya safari ile. Ikanibidi kukaa tena na kumuelezea juu ya safari ile.
“Magugi hakufanikiwa kupata majibu juu ya ukweli wa habari alizozipata kuhusu Sauda kutoka kwa majini wake kama ambavyo amekuwa akipata kabla, pengine ndiyo matunda ya safari ya mlima Kalingisi” Alizungumza mzee yule na kisha akaongeza “Magugi ameamua kuwa kesho atamtumia mtabiri wake wa siku nyingi, mzee Mikausho ili amwambie hatua ambazo atapaswa kuchukua juu ya Sauda, mnaweza kwenda, huo ndo msaada pekee ambao naweza kuwapa” alimaliza kuelezea mzee yule nami sikutaka kuendelea kuwa kero, nikaaga na kuondoka na kijana yule.
“unapafahamu kwa mzee Mikausho?” nilimuuliza kijana yule naye akakiri kupajua, na safari ya kwenda huko ikaanza mara moja…

usikose sehemu ya 41


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here