SHARE

Usiku wa Kitendawili unaotarajiwa kufanyika Disemba 8 mwaka huu huko mkoani Dodoma ndio habari ya mjini kwa sasa, kwani watanzania wanashahuku kubwa ya kusikia kauli za viongozi mbalimbali wastaafu na walioko madarakani kuhusu harakati za Tanzania kupata uhuru pamoja na jinsi watanzania walivyounganika na kuwa kitu kimoja licha ya kuwa na makabila takribani 120.

Viongozi wa zamani wa serikali, walipo madarakani pamoja na wadau wakiwa wamekaa chini kwenye mikeka ya asili na vigoda watapata fursa ya kueleza namna serikali kupitia viongozi wake ilivyoweza kuondoa mambo ya ukabila ambayo yanayatesa mataifa mengi ya Afrika.

Akiongea na TBC katika kipindi cha Tanzania Mpya, Mrisho Mpoto amesema kuwa siku hiyo mgeni rasmi ambaye ni Rais John Pombe Magufuli atapata fursa ya kueleza maisha yake ya utoto na namna alivyoweza kusimama katika mstari ambao kila mmoja kwa sasa akiangalia matendo yake anaona rais kweli ni mzalendo wa kweli.

“Usiku wa Kitendawili ni ukurasa mpya wa kujifunza mambo mapya kuhusu uzalendo na kuanza utekelezaji mara moja, na kama unavyojua tutakuwa na viongozi mbalimbali katika huo usiku, Mhe. Rais wetu John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu pamoja na Waziri Mkuu na wote watapata fursa ya kueleza mawili machache kuhusu uzalendo, wao waliwezaje kuwa wazalendo wa kweli, tunapokuwa kuna jambo la kitaifa tuungane kwa pamoja kama watanzania, wanapotokea watu wachache wakajitenga huo sio uzalendo ndio maana nikasema hiyo siku tutamsikiliza Rais wetu amewezaje kuwa mzalendo ambaye kila mtu akimuangalia anaona kabisa huyo ni mzalendo na apaswa kuungwa mkono na watanzania wote kwa manufaa ya taifa leo na la kesho,” alisema Mpoto.

Aliongeza, “Lakini pia tumeomba protocol zisiwe kali sanaa kwa upande watanzania na viongozi ili watu wafunguke, tunataka Rais wetu atuambie kwanini yupo vile, kwa nini anakuwa na uchungu na watanzania hasa watanzania wa chini, kwa nini anawafikiria wanyonge zaidi.

Kuna wakati Mhe Rais anasema Tanzania ya Viwanda watu wanaona kama haeleweki, lakini sasa hivi viwanda vimeongezeka kila mtu amenza kuamini kwamba Tanzania ya Viwanda inawezekana, kwa sababu imetoka kwenye ubongo kama wazo imeenda kwenye uhalisia.

Kwahiyo ninachosema kwamba tutakaa kwenye mikeka na vigoda, tutakula ugali ya muhogo, kisamvu na madafu , Majaliwa pale, Mama Samia pale , tunakaa pale na ule ukumbi umetengenezwa kama kuna vijiji na mitaa, Mhe atapita pale kwenda kusalimia kijiji cha jirani watuambie tu wamewezaje kuondoa suala la ukabila, nchi za wenzetu wanapigana kila siku, kwahiyo kama tukitumia nguvu iliyotumiaka kuwaonganisha watanzania ambao kwa wingi wetu tuna makabila 120, lakini wote tukawa kitu kimoja kwanini tushindwe watanzania na wote tuimbe wimbo mmoja wa Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’,”

Mpoto amesema kwa sasa kuna haja ya kuwa na nyimbo za hamasa ambazo zitawajenga watanzania kuwa wazalendo na kukataa rushwa pamoja na kuacha kufanya kazi kizembe.

Usiku wa Kitendawili umeanzishwa na msanii wa huyo wa muziki wa asili nchini baada ya kuachia wimbo wake ‘Kitendawili’ na baadaye kufikiria kuanzisha usiku wa wimbo huo kwaajili ya kuwakutanisha wadau na kujadili kuhusu Uzalendo.

Alisema baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo, itayokuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julis Kambarage Nyerere, wataanza kuzungumza katika mikoa mbalimbali kupaza sauti kuhusu uzalendo.

Mpoto alisema mambo yatayopambaniwa katika kampeni hiyo ni pamoja na kudhibiti na hatimaye kukomesha kabisa mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma, kupunguza tuhuma za rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma pamoja kuongeza hari ya kufanya kazi na Uzalendo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here