SHARE

WASANII wa muziki wakiongozwa na msanii wa Muziki wa Asili, Mrisho Mpoto wameandaa wimbo maalumu ambao utaimbwa Usiku wa Kitendawili katika uzinduzi wa Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ inayotarajia kufanyika siku ya kesho huko mkoani Dodoma.

Kampeni hiyo itazinduliwa na Rais, Dk. John Pombe Magufuli na baada ya hapo itazunguka katika mikoa mbalimbali nchini kuhamasisha masuala ya Uzalendo.
Akiongea na waandishi wa leo, mmoja kati ya waratibu wa kampeni hiyo, Mrisho Mpoto amesema wimbo huyo umeandaliwa na wasanii wengi akiwemo Witness ‘Kibongwe Mwepesi’ pamoja na wasanii wengi lukuki waliojaliwa vipaji.

“Wasanii kama wasanii tuliona tukae chini tuandae wimbo kuonyesha suala la uzalendo ni kitu muhimu kwa ustawi wa taifa, bila uzalendo hakuna amani. Tuunge juhudi za rais wetu Magufuli kwa sababu ameonyesha kwamba yeye ni mzalendo wa kweli na anaweza kufanya mambo makubwa kwa ajili ya Watanzania wa chini,” alisema Mpoto.

Kampeni hiyo ya kitaifa itakuwa ikifanyika kila mwaka sambamba na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere.

Kwa upande wa Witness amesema anajisikia fahari kuimba uzalendo kwa ajili ya nchi yake na kudai kuwa wimbo huo utaenda kufungua fikra za Watanzania wengi kuhusu Uzalendo wa nchi yao.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here