SHARE

Story: Mpaka Kieleweke

SEHEMU YA 41

Ilipoishia….

“Magugi ameamua kuwa kesho atamtumia mtabiri wake wa siku nyingi, mzee Mikausho ili amwambie hatua ambazo atapaswa kuchukua juu ya Sauda, mnaweza kwenda, huo ndo msaada pekee ambao naweza kuwapa” alimaliza kuelezea mzee yule nami sikutaka kuendelea kuwa kero, nikaaga na kuondoka na kijana yule.
“unapafahamu kwa mzee Mikausho?” nilimuuliza kijana yule naye akakiri kupajua, na safari ya kwenda huko ikaanza mara moja…

Endelea…

njiani kote nilikuwa nikiwaza nakwenda kuongea nini na mzee Mikausho, jibu la swali hilo lilionekana kuwa mbali sana kwa wakati huo lakini bado ilikuwa lazima niende kwa maana kutokwenda ilikuwa ni kuruhusu kifo cha Sauda na kisha mipango yote kuvurugika. “haya ni mayai ya bundi wa zamani sana, mayai haya ni muhimu sana kwenye shughuli za uchai.. mchawi yuko tayari kufanya jambo lolote lililo ndani ya uwezo wake iwapo mayai haya yatakuwa malipo” maelezo yale ya Mnaro yalipita ghafla kichwani mwangu kama vile kuna mtu alikuwa akinielezea.

“inatubidi kurudi kwanza mpaka nyumbani kabla ya kwenda kwa mzee Mikausho” Nilimuelezea kijana yule, akaonesha kushangazwa na wazo lile hata akauliza “kwanini turudi kwanza nyumbani? unajua ni karibia saa tano sasa?” ilikuwa lazima kurudi nyumbani kwa maana sikuwa na ule mkoba alionipa Mnaro na sasa niliamini kuwa kuna kitu muhimu sana kwa wakati ule kiko ndani ya mkoba ule.. “ni bora kufanya mambo polepole lakini kwa usahihi kuliko kuwa na haraka isiyo na mafanikio, turudi” nilisema kwa msisitizo na kijana yule akawa mtiifu na safari ya kurudi penye makazi yetu ikaanza.. “vijana wa umri wangu huku Muifufu hawajui kama kuna maisha mengine ambayo yaliwastahili na sio haya” alivunja ukimya kijana yule na kuanzisha mazungumzo tukiwa katika safari ya kuelekea nyumbani.. “watu ambao walikuja Muifufu kwa hiari yao wote ni watu wazima kwa sasa, sisi mama zetu walipewa adhabu ya kuja huku kwakuwa walikuwa na mimba zetu matumboni mwao” alielezea kijana yule akionesha kuumizwa sana na hali ile.. niliuona uchu wa kuyataka maisha ya dunia ya kawaida ambao alikuwanao waziwazi kijana yule.

“umewahi kumuona mama yako?” nilimuuliza kijana yule jambo ambalo lilionekana kumuongezea machungu “mama yangu na wanawake wengine wote ambao huporwa maisha yao na kuletwa Muifufu kwaajili ya kujifungua watoto wao ili kuijaza Muifufu hufa mwezi mmoja baada ya kujifungua!.. hivyo mama yangu alinilea kwa mwezi mmoja tu kabla ya kufariki kwake” alieliza kijana yule. “mwisho wa Magugi umekaribia, ni lazima aadhibiwe kwa uonevu ambao amekuwa akiufanya” nilisema kumfariji kijana yule..
“sitokuwa na furaha maishani mwangu mpaka ambapo nitayatoa maisha ya Magugi kwa mikono yangu mwenyewe” alisema kijana yule akiongea kwa usongo wa hali ya juu huku aking’ata mengo yake kwanguvu kuonesha hasira alizokuwanazo”, sasa nikaamua kubadilisha mada kwa maana niliona mada ile ilikuwa ikimuumiza sana kijana yule.. “unajua mpaka sasa sikujui jina lako, unaitwa nani?” niliuza ili kubadili mada.

“naitwa Hisham” alijibu kwa kifupi kijana yule.. “Hisham unaweza kuwa unajua ambapo wanawake wajawazito huwekwa baada ya kukamatwa na kuletwa Muifufu?” Niliuliza tena nikilenga kujua alipo mke wangu kwa maana nilihitaji sana kumuona..
“kuna jumba moja kubwa sana, huwa wanahifadhiwa humo wakipewa huduma zote ili wawe na afya njema na kujifungua salama” alielezea kijana yule nami nikapata hamu kubwa ya kufika kwenye jumba hilo..
“tumalizane kwanza na hili, kesho utanipeleka kwenye hilo jumba”. Tulikuwa tumefika pale nyumbani, nikaingia ndani na kuchukua ule mkoba wa Mnaro na kutokanao kisha safari ya kwenda kwa mzee Mikausho ikaanza tena.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here