SHARE

Ulikuwa ni mwendo wa kama dakika ishirini tukawa tumefika kwenye nyumba moja kubwa na kubisha hodi kwa kama dakika tatu bila majibu “bila shaka watakuwa wamelala tayari” alisema Hisham!.. “lazima tuongee naye, hata kama amelala lazima tuhakikishe anaamka” tukaendelea kugonga mlango ule, mara tukasikia ukifunguliwa.. “shikamoo mzee Mikausho” Hisham alimsalimia mzee ambaye alikuwa amefungua mlango akiwa na taa ya chemli mkononi mwake.

“marahaba Hisham” aliitikia mzee yule. Inaonekana mzee Mikausho na Hisham walikuwa wakifahamiana vizuri tu.. “shikamoo mzee” na mimi nikasalimia, mzee Mikausho akaitikia na kugeuza kurudi ndani “karibuni vijana” mzee Mikausho alikuwa mzee sana, hata mwendo wake ulikuwa wa kuinama.
Tukaingia ndani mzee Mikausho akiwa ametangulia huku sisi tukimfuatia nyuma yake.

Tukaishia sebuleni ambapo tulikaa na mzee Mikausho akafungua maongezi “watu ambao tunaelewa nini kinaendelea Muifufu ni wachache mno, ni ambao akili zetu ziliacha zikiwa nzima kwa sababu maalum” aliongea mzee Mikausho na kunifanya nijue kuwa alikuwa ana kitu ambacho anafahamu juu ya ujio wetu. “mimi niliachwa kuwa sawa kwaajili ya uwezo wangu wa kutabiri mambo yajayo pamoja na kuganga magonjwa mbalimbali” alisita kuongea mzee yule, akatulazama kwa zamu kisha akasema akiniangalia mimi “tuna mengi ya kuongea, lakini hatuna muda, sasa nipatie mzigo ambao umeniletea” alisema mzee yule akiniacha mdomo wazi, aliwezaje kujua kama nilileta kitu kwaajili ya kumpa?..
“inatupasa kuongea kwanza na kukubaliana kabla ya kukupatia huo mzigo” nilionesha nia yangu ya kufanya makubaliano kabla ya kutoa malipo ya jambo ambalo alipaswa kulifanya..

“mimi ndiye nisemaye nini kinafanyika, sio wewe! nipatie huo mzigo haraka na muende mkalale” alisema kwa kufoka mzee yule nami nikatii haraka sana!, nikatoa yai moja la bundi na kumkabidhi..

“haya nendeni mkalale, niachieni mimi jambo hili” aliamuru mzee yule mimi na Hisham tukatazamana na kusimama, tukatembea kuelekea ulipo mlango wa kutokea huku mzee Mikausho akitufuata kwa nyuma kutusindikiza. Hisham ambaye ndiye aliyekuwa mbele akafungua mlango na kutangulia nnje mimi nikifuatia.. “hongera sana kwa kazi nzuri kule Mlima Kalingisi, umenirahisishia sana” alisema mzee yule huku akifunga mlango nasi tukaendelea na safari ya kwenda nyumbani ambapo tulifika na kupumzika..

Asubuhi niliamka mapema na kumkumbusha Hisham juu ya safari ya kwenda ambapo wanahifadhiwa wajawazito pengine ningemuona mke wangu.
“sasa inabidi ungoje nikaongee na ambao wana zamu ya kupeleka kuni au maji leo niwaombe watuachie sisi kazi hiyo, pia nikakutafutie sare kama hizi zangu maana bila kuvaa hizi utashtukiwa haraka sana” alisema Hisham nami nikamkubalia, akaondoka akiniacha nikichimba mihogo ambayo ilikuwa imepandwa pale nyumbani kwaajili ya kuandaa kifungua kinywa..

Baada ya muda Hisham alirudi akiwa ameongozana na kijana mwingine ambaye nilimtambua moja kwa moja kuwa ni mwenzie ambaye walinisindikaza naye wakati nakwenda Mlima Kalingisi, na hata jana yake niliwakuta pamoja pale shamba nikitokea Mlima Kalingisi.

Walikuwa wamebeba mabegani mwao madumu mawili ya majini yakiwa yameunganishwa na mti mgumu dumu moja likiwa mbele na lingine likiwa nyuma ya mti ule ambao ulikaa begani vizuri.
Vijana wale wakanywa chai kwa mihogo niliyokuwa nimeandaa kisha nikapewa sare na kuzivaa na ikapangwa safari ya mimi na Hisham kuelekea mtoni kuchukua maji na kisha kuyapelekea kwenye lile jumba ambalo alikuwepo mke wangu..


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here