SHARE

MREMBO mmoja wa nchini Iran, Sahar Tabar, aliyedaiwa kufanyiwa upasuaji wa sura mara 50 akitaka afanane na nyota wa filamu nchini Marekani, Angelina Jolie, amedaiwa kuwa anaweza kufariki dunia kutokana na njaa.

Sahar, mwenye miaka 19, kutoka mjini Tehran, ambaye anadaiwa kuwa shabiki mkubwa wa mwigizaji huyo aliyecheza filamu ya Tomb Raider, aliweka picha zake kwenye mtandao wa Instagram zikimwonyesha kuwa na sura tofauti na ilivyokuwa zamani.

Kwa mujibu wa mtandao wa Ubelgiji, Sud Info, Sahar anadaiwa kufanyiwa operesheni hizo zote ndani ya miezi michache, lakini mrembo huyo anashutumiwa na mashabiki wake kutumia kamera za kompyuta ili kufanya sura yake ionekane kama ya Angelina wakikataa kuamini kama amefanyiwa upasuaji.

“Siamini kama amefanyiwa upasuaji, inaonekana kama amefanya ‘makeup’ kutumia kamera ya kompyuta ili aonekane kama sura aliyonayo sasa,” alisema mchambuzi mmoja.

Lakini mwenyewe amesema anaweza kufanya lolote ili ahakikishe anafanana na nyota huyo wa Marekani, ingawa baadaye alionekana kuwa tofauti kwenye mtandao wake wa Instagram na mashabiki wake kwenye mtandao huo kusema kuna mchanganyiko wa kutengenezwa kutumia kamera ya kompyuta na ‘make-up’ bab kubwa.

Je, ni kweli Sahar anatumia picha za kompyuta kubadilisha mwonekano wa sura yake au sura yake ya zamani ikoje?

Msichana huyo aliyezaliwa Februari mwaka 1998, amekuwa kwenye kazi kubwa ya kupangilia vyakula vyake ili kupunguza uzito hadi kuwa kilo 40, huku harakati zake za kutaka kufanana na Angelina Jolie zimemfanya abadilike sura na kupachikwa jina la ‘Zombie’ na mashabiki wake wa Instagram.

Kabla ya kufanyiwa upasuaji, Sahar alikuwa msichana mwenye sura ya kawaida, macho yake ya rangi ya kahawia na kope za rangi ya kahawia zilizochongwa, lakini sasa anavaa miwani ya rangi ya bluu ya bahari akiwa na midomo mikubwa ‘lips) na pua iliyochongoka.

Mashavu yake yakionekana kubonyea zaidi, akiwa na vipini kwenye mashavu yake yote mawili, huku pua yake ikionekana kupinda tofauti na ile ya zamani.

Daktari wa mrembo huyo aliyemfanyia upasuaji, Michael Salzhauer, anathibitisha kile kinachowatia shaka mashabiki wa Sahar kwamba ni kweli amefanyiwa upasuaji au la, akiuambia mtandao wa Newsweek mwishoni mwa wiki iliyopita, akianza na kuzungumzia muundo wa pua, akisema: “Kuna upandikizaji wa madini ya silicone ili kuiinua pua na kuisaidia kusimama vizuri.”

“Kwa upande wa midomo ‘lips’ imejazwa na nyama ya nyongeza na kufanyiwa utaratibu wa kuinua ‘lips’ hizo na kuonekana nyekundu kwenye sehemu ya mbele ya ‘lips’ hizo,” anasema Salzhauer, ambaye ni Mkuu wa kitengo cha upasuaji kwenye Hospitali ya Upasuaji ya Bal Harbour mjini Miami nchini Marekani.

Salzhauer, ambaye amehusika kwenye upasuaji huo, amesema mrembo huyo anahitaji msaada wa haraka. “Mwanamke huyu anahitaji kuwekwa hospitali na kulishwa kwa mpira kumwongezea madini ya protini na kufanyiwa ushauri wa masuala ya akili ama anaweza akafa kwa njaa,” alisema daktari huyo.

Credit – Bingwa


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here