SHARE

Kazi ya kubeba maji yale ilikuwa ngumu sana, ule mti ulikuwa ukiumiza mabega vibaya, ni bora maji yale ningeyabeba mikononi kawaida kwa maana nimewahi kubeba mara nyingi tu lakini aina hii ya ubebaji ilikuwa mpaya kabisa. Tulifika kwenye jumba lile nikiwa hoi, tukamimina maji kwenye moja ya mapipa makubwa yaliyokuwepo kwenye eneo ambalo kwa harakaharaka lilionekana kuwa la jikoni, kisha tukaelekea kwenye eneo ambalo lilikuwa na uwanja mkubwa sana watu wengi wakiendelea na shughuli zao, mara nikapishana na binti ambaye niliitambua sura yake haraka, nikaingiza mkono mfukoni na kutoa picha ambayo nilikuwa nimekwenda nayo na kujaribu kufananisha sura ambayo ilikuwepo kwenye picha na ile ambayo niliiona pale, hakika huyu alikuwa ni Regina, binti yake bwana Waisaka (yule hakimu ambaye alinitaka kuhakikisha ninatoka Muifufu nikiwa na binti yake).

Sikutaka kupoteza muda sana kwa binti yule, jambo la maana ni kuwa nilikuwa nimejua alipo, sasa kazi ya kumtafuta mke wangu ikaendelea!, Hisham alikuwa amenipotea baada ya mimi kuwa makini na picha ile kujaribu kuifananisha na mtu ambaye nilimuona..

Nikaendelea kuangalia bila mafanikio, lakini mara Hisham akanijia kwa kasi “njoo huku nimemuona”
alinieleza kwa kunong’ona huku yeye akigeuka na kutangulia nami nikamfuata haraka mpaka eneo ambalo lilikuwa limejitenda, nikamkuta mke wangu akiwa amekaa juu ya ngozi ya mnyama chini ya mti wa kivuli. Hisham akaniacha pale na kupotela ambapo sikupajua.

Nilimtazama kwa mbali kwa dakika kama tatu, kisha nikaamua kusogea mpaka pale alipokuwa amekaa, mke wangu alinitizama usoni lakini hakuonesha mshtuko wowote jambo ambalo lilinishangaza. “habari yako dada?” nilimsalimia mke wangu kama watu ambao hatujuani, naye akaitikia “nzuri tu kaka, sijui wewe”…
hali ile iliniumiza sana, mke wangu alikuwa hanijui kabisa kama ambavyo nilikuwa nimetahadharishwa kabla..

“sijui unaitwa nani dada yangu?” niliuliza kujaribu kuona alikuwa hajitambui kwa kiasi gani.. “mimi naitwa Victoria, wengi wanapenda kuniita Vicky, alijibu mke wangu huku akiachia lile tabasamu lake zuri ambalo nilipenda kuliona usoni mwake siku zote.

Roho iliniuma sana, nikatamani kumrudisha mke wangu kwenye himaya yangu wakati huohuo lakini nikakumbuka kuwa sikuwa na lakufanya zaidi ya kuyafanya mambo kwa kasi ambayo mambo yenyewe yalitaka kwendanayo ili nisije nikaharibu kila kitu.
“yani wewe baadala ya kwenda kufuata maji unaleta umalaya hapa?” nilishtuliwa na sauti iliyotoka nyuma yangu, nikageuka na kukutana na mtu mwenye mwili mkubwa na ana jicho moja, nikabaki nimesimama nikimshangaa bila kusema neno lolote!

“kwenda kachukue madumu ukalete maji” liliamuru jitu lile kubwa na mimi nikaondoka haraka eneo lile huku yeye akifuata nyuma yangu “watu wengine mnatafutaga kufa tu, unaingia hadi anga za mzee? mzee ana mpango naye yule” alisema kimzaha bwana yule nami nikajifanya kama ambaye sikuwa nikiyatilia maanani maneno yale, kumbe nilikuwa nikiyasikiliza kwa makini sana. Nikaenda mpaka eneo la jikoni ambako nilimkuta Hisham akichukua madumu yake na mimi nikachukua yangu, kisha tukatoka “fanyeni kinachowaleta humu mabwana, acheni ujinga” alitusindikiza na maneno bwana yule, nadhani alikuwa mlinzi , sisi tukaendelea na safari ya kwenda nnje bila kusema lolote.

“mzee ana mpangonaye yule? inamaana ni kweli Magugi anataka kumuoa mke wangu?” nilizungumza kwa sauti baada ya kuwa tumetoka kabisa kwenye lile jengo..
“ndivyo inavyosemekana, Magugi ana mpango wa kumuoa mkeo” alichangia Hisham..
“lakini si ulisema wanawake wale huwa wanauwawa baada ya kujifungua?” niliuliza.

“ni kweli, lakini sidhani kama sheria hiyo itatekelezeka kwa mwanamke ambaye anampenda” alijibu Hisham.
“hilo halitotokea kamwe, labda ayatoe maisha yangu kwanza” nilisema na safari yetu ikaendelea. Sikuwa nikitamani kwenda tena kwenye shughuli ile ya kuchota maji kwa maana lengo la safari ile lilikuwa limetimia tayari..

“sasa warudishie wale mabwana kazi yao waendeleenayo, mimi nakwenda kupumzika bwana” niliagiza na Hisham akaelekea kwenye utekelezaji wa hilo na kuniacha nikielekea nyumbani kupumzika.

Nilifika nyumbani, nikazunguka nyuma ya nyuma na kuoga, maana hakukuwa na choo wala bafu kwenye nyumba ile.
Nilipomaliza kuoga nikakaa pale nnje nikingojea maji yakauke mwilini ili niende kulala, lakini mara nilimuona Hisham akija mbio…
“watu wanakusanyika kwenye uwanja wa kwa Magugi, Inasemekana hukumu ya bi. Sauda inatolewa” habari ile ilikuwa yakushtua sana kwangu kwani nilikuwa naamini kuwa swala lile lilikuwa limeisha..
“inamaana mzee Mikausho amefanya uhuni?” niliuliza sw ali ambalo hakuwepo mwenye jibu lake pale, huku nikiingia ndani kuchukua shati na kutoka kwa kwasi nikiongozana na Hisham..

Usikose sehemu ya 44


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here