SHARE

Waziri wa zamani wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Gaudencia Kabaka amechaguliwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) kumrithi Sofia Simba aliyeondolewa kabla ya muda wake.

Kabaka alichaguliwa kuwa Mwenyekiti UWT kwa kipindi cha miaka mitano kwa kura nyingi na wajumbe wa mkutano mkuu wa UWT. Akitangaza matokeo hayo mjini Dodoma jana, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi UWT, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Hadija Abood alimtangaza Kabaka ndiye ameshinda wa nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 636.

Aliwataja wagombea wengine waliogombea nafasi hiyo ambao kura hazikutosha kuwa ni Ngollo Malenya aliyepata kura 31, Dk Juliana Manyere (24), Sophia Mpumilwa (24) ambao kwa pamoja wamepata jumla ya kura 79.

Msimamizi huyo wa uchaguzi pia alimtangaza Thuwaybah Kissasi kuwa Makamu Mwenyekiti wa UWT kwa kupata jumla ya kura 385. Msimamizi huyo pia alimtaja mshindi wa nafasi ya Uwakilishi Jumuiya ya Wazazi ni Dk Zainab Gama aliyepata kura 482 na mwakilishi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) ni Khadija Taya Keisha aliyepata kura 532.

Wajumbe wa Baraza Kuu Zanzibar na Tanzania Bara walioshinda ni Grace Kingalame 547, Dk Alice Kaijage (505), Neema Mwandabila (484), Anna Msuya (284) na Lucy Mwanisawa (256).

Wengine ni Nadra Gulam Rashid aliyepata kura 406, Zainab Khamis Shomari (367), Hasina Shaibu Ame alipata kura 268, Asmahany Juma Ally alipata kura 265 na Lucy Mwakyembe (206).

Walioshinda kuwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) CCM ni Catherine Peter Nao (438), Asya Ali Khamis (347), Halima Okash (322), Mariam Mungula aliyepata kura 315 na Catherine Kitandula aliyepata kura 303.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Kabaka alisema anajivunia kuwa mwana CCM na jumuiya hiyo imeonesha mfano kwenye uchaguzi huo kwa kufanya uchaguzi kwa amani. “Jana Rais John Magufuli alitoa hotuba yenye maelekezo nasaha na mtazamo wa UWT anayoitarajia na akasema anataka kuiona UWT ya kina Sophia Kawawa, tutajitahidi kuirudisha ifanane na ya Sophia Kawawa na Anna Abdallah,” alisema Kabaka katika hotuba yake.

Aliomba ushirikiano na kusema kazi inaanza kwa kuwatembelea wananchi na wana CCM kusikiliza kero zao zifanyiwe kazi na Serikali. “Mwaka 2019 tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, 2020 Uchaguzi Mkuu na tuna uchaguzi mdogo mwingine, tuanze maandalizi sasa kwa ajili ya uchaguzi huo,” alisema Kabaka.

Akifunga mkutano huo, Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu aliwatahadharisha kuwa kuna watu waliitwa na kupewa maelekezo lakini Rais Magufuli alisema hakuna aliyepewa maelekezo hivyo wachague viongozi bora.

Samia alisema katika uchaguzi hutokea makundi na kutaka yavunjwe wakafanye kazi inayotarajiwa na chama, CCM kutoka kwao. Aliwataka waisimamie Serikali ili iweze kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuwa hatua hiyo itampa nguvu katika utendaji kazi wake.

“UWT ya kina mama Sophia Kawawa ilisimamia Serikali, sasa tukasimamie haya,” alisema. Kabaka ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Kabaka anachukua nafasi ya Sofia Simba aliyekuwa amefukuzwa uanachama kwa kukosa maadili, lakini amerudishwa kundini baada ya kuomba msamaha na Rais Magufuli akaomba ridhaa ya wajumbe wa NEC CCM kumsamehe.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here