SHARE

Ilipoishia….

mara nilimuona Hisham akija mbio…
“watu wanakusanyika kwenye uwanja wa kwa Magugi, Inasemekana hukumu ya bi. Sauda inatolewa” habari ile ilikuwa yakushtua sana kwangu kwani nilikuwa naamini kuwa swala lile lilikuwa limeisha..
“inamaana mzee Mikausho amefanya uhuni?” niliuliza sw ali ambalo hakuwepo mwenye jibu lake pale, huku nikiingia ndani kuchukua shati na kutoka kwa kwasi nikiongozana na Hisham..

Endelea..

Tulikwenda moja kwa moja mpaka kwenye uwanja mkubwa mbele ya nyumba ambayo niliikumbuka kuwa ilikuwa ile nyumba ya Magugi, ingawa sikufanikiwa kupaona niliporudi tena.
Kwenye uwanja ule kulikuwa kumekusanyika watu wengi mno na mara nikamuona Sauda akiletwa mbele ya umati ule akiwa chini ya ulinzi wa wanaume wawili walioonekana waziwazi kuwa wakatili hasa, minong’ono ikatawala wakati akisogezwa mbele ya umati ule.
Baada ya watu wale kumfikisha ambapo walikusudia walimsukuma akaanguka chini na kutulia magoti, kisha mzee Magugi mwenyewe akasimama kutoka katika kiti cha thamani alichokuwa amekalia akinyoosha mkono wake wa kulia juu kuashiria kuunyamazisha umati ule uliokuwa umezi disha minong’ono, kimya cha kutisha kikatokea mara moja na Magugi akaanza kuzungumza.

“Leo tuko hapa kushuhudia kuwa sheria ni msumeno!” alianza kuongea Magugi ambaye alikuwa na sauti iliyojaa ukali na ukosefu wa huruma.. “hakuna mtu hata mmoja ambaye anaweza kuwa juu ya sheria zangu na mfano mtauona muda mfupi ujao. Huyu mwanamke ni msaliti, amekuwa akifanya mambo mengi nyuma ya mgongo wangu akidhani haonekani ila serikali yangu ina mkono mrefu sana” Aliendelea kuongea Magugi akiwa amesimama hatua chache mbele ya kiti chake huku viti vya nyuma yake vikiwa vimekaliwa na watu wengine sita, niliweza kuwa tambua watu wawili tu kati ya sita ambao walikuwa wamekaa kwenye viti vilivyokuwa pale mbele!, walikuwa ni wazee ambao niliwatembelea majumbani mwao usiku kutaka msaada wa kuokoa maisha ya Sauda, hasira zangu zilikuwa juu ya mzee Mikausho ambaye aliahidi kutoa msaada lakini sasa alikuwa amekaa pale mbele kushuhudia kifo cha mwanamke ambaye aliahidi kumlinda. Kama wamefikia kuamua kumuua Sauda bila shaka ni ushauri wa mzee Mikausho, kwani utabiri wake ndio ambao ulikuwa ukisubiriwa ili kuamua Sauda aadhibiwe ama laah, kwa maana Magugi hakuwa na uhakika juu ya hili.

“Ili iwe fundisho kwa wengine, ninaku hukumu kifo cha kukatwa kichwa kwa upanga” alitamka Magugi, umati ule ukalipuka kwa kelele za kushangilia, ama kweli akili za watu wale hazikuwa sawa, siku zote walikuwa upande wa Magugi na kuona kila uamuzi wake ulikuwa sahihi. “hatuwezi kuruhusu Sauda afe!, inatupasa kufanya kitu” nilimwambia Hisham kwa sauti ya kunong’ona ikiwa na wasiwasi mwingi ndani yake.. “wewe ni mtu muhimu sana kaka, ukombozi wa Muifufu unakutegemea! tumia busara kwenye maamuzi ama utakata matumaini yote tuliyonayo, huu sio wakati wa kukata tamaa” alisema Hisham, maneno yake yakionesha ukakamavu wa hali ya juu. Nilimuele wa sana Hisham na kuamua kuwa mvumilivu na kushuhudia Sauda akifa bila msaada wowote kwani hata kama ningeamua kutoa msaada, ni nini ningefanya mbele ya watu wote wale? nikaamua kuwa mpole.

Wakati huu watu wale waliomleta Sauda walimburuza mpaka kwenye meza ndogo iliyokuwepo pale mbele wakaifunga mikono y ake kwa kamba ambazo zilishikanishwa vizuri kwenye meza ile huku paji lake la uso likigusa kwenye meza ile na kuacha sehemu ya nyuma ya shingo ikiwa tayari kwa kukatwa!..
Mtu mrefu sana aliyekuwa amevaa kinyago cha kuficha sura yake akasogea mpaka pale walipokuwa amefungwa Sauda akiwa na panga refu sana, maalumu kwaajili ya kuchinjia. Mtu yule alikuwa amesimama kama ambaye anangoja amri ya kutekeleza tukio lile la kinyama!.. umati wote ulikuwa ukipiga kelele nyingi huku zikisikika kauli za kuchochea kitendo kile kifanyike haraka!, hakika watu wale hawakuwa na huruma hata chembe. Magugi akanyoosha mkon o wake kuwanyamazisha kwa mara nyingine na watu wale wakatii.. “KATAAA” aliamuru Magugi na mtu yule akanyanyua panga juu kwa kasi tayari kwa kulishusha shingoni mwa Sauda!….
Niliishiwa nguvu mwili mzima ukawa ukinitetemeka na jasho jingi likinitoka.

Kabla panga lile halijashuka kulitokea tukio la ajabu sana..
ilitokea radi ambayo ilikwenda moja kwa moja na kupiga kwenye lile panga na kufuatiwa na kishindo kikubwa sana! panga lile likaponyoka mkononi mwa bwana yule na kuanguka mbali..
watu wote wakawa kimya wakishangaa kilichotokea.. “mfungueni, hana hatia” alisimama na kusema mzee Mikausho, kisha akaendelea “siku zote palipo ukweli, uongo hujitenga! mwanamke huyu hana hatia ndio maana mizimu ya mababu imezuia adhabu hii na kuipinga ni kukaribisha matatizo makubwa” alielezea mzee Mikausho.

Itaendelea sehemu ya 45


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here