SHARE

Sauda akafunguliwa na kunyanyuliwa akasaidiwa kutembea kuelekea ndani ya jumba la Magugi, Magugi mwenyewe akifuata kwa nyuma.
“tawanyikeni, tutawajuza ambacho kitaendelea” alizungumza mmoja wa wazee ambao walikuwa wamekaa kwenye viti pale mbele kisha wazee wale wakaanza kuingia kwenye jumba la Magugi h uku watu wakitawanyika..

“mimi sio mtu wa kuvunja ahadi. Nimeona jinsi ambavyo umekuwa ukiteswa na dhana ya kuwa nimefanya usaliti” alisema mzee Mikausho ambaye alikuja mpaka ambapo nilikuwa nimesimama.. “kilichotokea hapa ni kazi ya la bundi ambalo ulinipa, kupitia yai hilo pia nitahakikisha nakuwa wa kuaminiwa na Magugi na watu wote wa Muifufu, kisha kazi itakuwa rahisi sana” alisema mzee yule kisha naye akaelekea kwenye jumba lile la Magugi. Nami nikaona sikuwa na sababu nyingine ya kunibakisha eneo lile, hivyo nikamtaka Hisham tuondoke.

Tukarudi kwenye makazi yetu tukiwa na matumaini mapya, moyo wangu ulikuwa ukimshukuru sana Mungu kwa kunusuru maisha ya Sauda.
Siku hiyo ilikwenda ikiwa tulivu mpaka giza lilipoanza kuingia ambapo nilimtaka Hisham tutoke kidogo ili nipate kuiona Muifufu inakuwaje usiku.
Tukatoka na kutembea huku na huko nikiona mambo mengi ya ajabu.

Watu wa Muifufu walikuwa ni wachawi sana na kwao halikuwa jambo la kuficha kama ambavyo uchawi umekuwa ukifichwa kwenye maisha ya dunia ya kawaida..
Watu wa Muifufu walikuwa wakifanya kazi nyingi usiku kuliko mchana, tena kwa njia za kichawi.
Nikafikia kutamani na wachawi wa dunia yetu wangekuwa kama hawa, wanatumia uchawi wao kufanyia kazi zao lakini sio kuleteana matatizo.

Niliona pia wachawi wakiendesha wanyama mbalimbali kama vyombo vya usafiri, wanyama wengine hata sikuwa nikiwajua, wengine walitisha sana hata kushindwa kuvumilia na kushtuka waziwazi wanapotokea mbele yangu.. ingawa Hisham alikuwa akinitaka kuvumilia kwa maana kushtuka kwangu kunaweza kusababisha kugundulika kuwa mimi sikuwa mwenyeji wa Muifufu kwa maana wanyama wale hawakuogopwa hata na watoto..
Nilichoshwa na safari ile kumwambia Hisham turudi nyumbani.
Tulipofika nyumbani tukamkuta yule kijana mwingine ambaye alinisindikiza pamoja na Hisham wakati wa safari ya kwenda mlima Kalingisi “nimewasubiria kwa muda sana, Sauda anataka kuonana na wewe” alinieleza kijana yule, akanitaka kufuatana naye nami nikafanya hivyo.

Tukaenda tukipita njia ambayo inakwenda kwa Magugi lakini kwa mara nyingine tulipofika eneo lile sikuiona nyumba ya Magugi..
“hapa si ndipo ilipokuwa nyumba ya Magugi? mbona haipo tena?” safari hii nilimuuliza kijana yule ambaye nilikuwa nimeongozana naye, naye akanijibu, “nyumba ya Magugi imefanyiwa zindiko la kumkinga na wabaya wake, hivyo ukiwa na nia mbaya naye kuwezi kuiona nyumba yake” alizungumza kijana yule. “lakini mbona mchana niliiona?” niliuliza baada ya kushindwa kuzielewa kanuni ambazo alikuwa akinikaririsha kijana yule.”kwasababu ni yeye aliyeitisha mkutano” alijibu kwa kifupi kijana yule tukawa tumefika kwenye nyumba ndogo lakini nzuri, tukaingia moja kwa moja ndani na kukaa kwenye viti, baada ya dakika kama tatu Sauda alikuja, akajumuika nasi na mazungumzo yakaanza.”hongera kwa safari ya mlima Kalingisi, imekuwa ya mafanikio na imetusaidia sana. Sasa tunaweza hatu kutumia uchawi ambao tunaujua kufanya mambo ambayo yako kinyume na Magugi bila hofu ya kukamatwa, lakini pia umefanya jambo la maana sana kumleta mzee Mikausho upande wetu, kwani ni mtu muhimu sana kwa sasa, Magugi anamuamini na kumsikiliza sana” alipongeza Sauda nami nikashukuru.. “asante pia kwa kuokoa
maisha yangu, kama sio jitihada zako ningekuwa nimekufa” alisema Sauda, akionesha hisia kali zilizokaribia kumtoa machozi.. “usijali, ilikuwa lazima uishi ili tuweze kufanikisha zoezi ambalo limenileta huku, siwezi kukwama kwenye kumuokoa mke wangu” niliongea kwa msisitizo.

“kwa msaada ulionipa leo, nitahakikisha mkeo anarudi duniani kwa gharama yoyote” alisema Sauda nami nikashukuru.
Sasa kazi imebaki ndogo tu, inatupasa kuiba ufunguo wa Kufungua mlango wa Muifufu kurudi duniani, jambo ambalo nakutegemea wewe kulifanya, mimi natakiwa kuwarudishia kumbukumbu zao wote ambao tutaondoka nao kwenda duniani, vinginevyo haitokuwa kazi rahisi kuwachukua” alielezea Sauda.
“ni lazima mimi ndio nikafanye kazi hiyo ya kuiba ufunguo? kwani hatuwezi kupata mtu ambaye yumo ndani kwa Magugi tayari?” niliuliza.

“Haya ni maelekezo ya mzee Mikausho, ametabiri mafanikio makubwa kwenye kukutumia wewe, utabiri wa mzee huyu haujawahi kukosea” alifafanua Sauda.
“itatuchukua siku ngapi kuondoka Muifufu, nimeyachoka sana maisha ya huku” niliuliza.
“mimi itanichukua siku tatu kuhakikisha akili za watu tunaowahitaji zinakuwa sawa na kumbukumbu zao zinarejea, baada ya hapo tutakuwa tunakutegemea wewe uibe ufunguo na kumuua Magugi” alielezea.

“hiyo funguo ikoje kwani, na Magugi huwa anaiweka wapi?” niliuliza kutaka kujua ugumu wa kazi yenyewe..
“hakuna anayeujua huo ufunguo zaidi ya Magugi mwenyewe, itakupasa kupeleleza sana” jibu hili likanifanya kuona kuwa kazi ile haikuwa ya kitoto.
“sasa nitaingiaje kwa Magugi?” Niliuliza tena..
“muda mfupi toka sasa mzee Mikausho atakuja kukuchukua hapa na kukupeleka yeye mwenyewe…

usikose sehemu ya 46


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here