SHARE

“Hukuja kufanya maisha humu ndani, kuna watu wamejitolea maisha yao na mpaka wakati huu wanateseka kwaajili yako, lakini hakuna kitu cha maana unafanya zaidi ya kuwa muhudumu, unadhani umebaki muda kiasi gani kabla mzee hajakugundua?” alihoji jini yule sauti yake ikishuka kidogo nami nikapata amani, nikashangaa kuona kuwa kiumbe yule ambaye nilikuwa nikimuhofia kumbe alikuwa upande wangu, nilishindwa hata kumwambia kama alikuwa na mchango mkubwa katiaka kushindwa kwangu mpaka wakati ule. “sijui hata pa kuanzia, kama kuna msaada wowote unaweza kunipa nitashukuru” nilimwambia jini yule kutaka kuona kama kulikuwa na namna yoyote ya kurahisisha kazi ile. Jini yule akanitupia ule mkoba wangu huku akisema “umepewa dhana zote za kukuwezesha kukamilisha hii kazi, ni uzembe wako tu”, jini yule akapotea ghafla kama ambavo alikuja na kuniacha nikiwaza namna ya kuharakisha kazi ile, nikavimwaga chini vifaa vyote ambavyo vilikuwemo kwenye ule mkoba na kuanza kujiuliza kipi kingeweza kunifaa kwenye kazi yangu, bado nilikuwa na yai moja la bundi, ile dawa ya kuzuia kupumua pamoja na ule mkate ambao niliambiwa nikifanikiwa kumlisha mtu ninaweza kumuamuru chochote na akafanya, akili yangu ikavutwa zaidi na ule mkate, nikaona kama nitafanikiwa kumlisha Magugi basi huenda jambo langu likawa jepesi, tatizo likawa namna gani nitamlisha Magigi mkate ule wa zamani tena umekauka mno, nikakosa jibu na kuamua kulala, haikuchukua muda nikawa usingizini.

Asubuhi na mapema nikaamka na kuendelea na majukumu yangu ya kila siku, akili yangu ikiwaza juu ya ndoto ambayo niliiota usiku, ndanoi ya ndoto hiyo nilimuona Mnaro aakinielekeza mambo mbalimbali, tukafikia kuliongelea swala la mkate ule ambao nilitaka kumlisha Magugi, Mnaro akanambia ndani ya ndoto ile kuwa mkate ule ulikuwa na uwezo wa kumpumbaza mtu akafanya kama ambavyo ningetaka afanye lakini ni ndani ya saa moja tu na baada ya hapo atarejea katika hali yake ya kawaida, nilikuwa nikijiuliza je ile ilikuwa ndoto tu kama ndoto nyingine au nikweli Mnaro alikuwa amenifikishia taarifa? Ndani ya ndoto ile Mnaro pia alinipa kafimbo kadogo na akaniambia mchwi akichapwa na fimbo ile huugua hadi kufa, hivyo akanitaka kuitumia silaha ile kwaajili ya kuyaondoa maisha ya Magugi,ila nilipoamka sikukaona kafimbo kale,hivyo nikaona labda ilikuwa ndoto tu.

Ulikuwa umekaribia wakati wa kumpelekea Magugi chakula cha mchana, nikapata wazo la kusaga kamkate kale ili niweze kupata ungaunga ambao nikiuchanganya kwenye chakula chake itakuwa ngumu kwa Magugi kugundua hivyo atakula chakula kile na mkate ule utampumbaza ili niweze kupata nafsi ya kumuhoji aweze kunielezea namna ya kufungua mlango wa Muifufu tuweze kurejea diniani, lakini nikajiuliza itakuwaje kama kweli nguvu ya dawa ile ingedumu ndani ya saa moja tu ikiwa sikuwa nimewaandaa waondokaji kwa safari, je muda wa saa moja ungetosha kuwaandaa na kuondoka kabla Magugi hajarudi katika akili yake na kutuzuia? Mwisho nikaamua kuwa inanibidi kuijaribu ile dawa kuona kama kweli nguvu yake itakaa ndani ya saa moja tu, pia nilitaka kujua kama dawa ile ina nguvu juu ya mchwi mkubwa kama Magugi, hivyo nikakagawe kamkte kale japo kalikuwa kadogo ili sehemu yake itumike kwa majaribio lakini ibakie sehemu ambayo itatumika kutimiza lengo halisi. Nikaenda haraka mpaka kule chumbani, nikauchukua mkoba wangu na kuanza harakati za kuutoa ule mkate. Lakini nilishangaa kukuta ndani ya mkoba ule kulikuwa na kafimbo kale ambacho niliota Mnaro kinikabidhi kwaajii ya kumuulia Magugi, nikkajikuta nikiamini kumbe ile haikuwa ndoto bali msaada wa Mnaro katika kufanikisha kazi ambayo ilinipeleka Muifufu, hivyo nikaachana haraka na wazo la kufanya majaribio ya mkate ule na baadala yake mawazo yangu yakahamia kwenye kufikiri namna ya kumfikia Sauda kumjulisha kuwa alitakiwa kuwaandaa watu kwa safari maana safari ilikuwa imetimia. Nikatoka na kwenda kumtafuta mzee Mikausho ambaye nilimuelezea kila kitu na kumtaka kutafuta namna ya kumfikishia Sauda ujumbe ule, naye akakubali.

Tulipanda kuwa kwa kutumia mkate ule wakati nampa Magugi chakula cha usiku, Magugi atapumbaa na kunipa nafasi ya kumuuliza namna ya kufungua mlango wa Muifufu kisha nitamchapa na fimbo ile naye atakufa kisha tutaufungua mlango ule kutumia ujuzi atakaokuwa amenipa Magugi kisha tutaondoka Muifufu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here