SHARE

JULAI 18, mwaka jana Abdulrahman Kinana aliandika barua ya kujiuzulu ukatibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ili kupisha mwenyekiti mtarajiwa wakati huo, Rais John Magufuli kupanga safu yake ya utendaji.

Ingawa uamuzi wa Kinana ni utamaduni uliojengeka ndani ya chama hicho wakati kikitoka kwenye mikono ya mwenyekiti mmoja kwenda mwingine, wachambuzi wengi wa kisiasa walichukuliwa kuwa huo ulikuwa mwisho wa enzi za uongozi wa kada huyo ndani ya CCM.

Lakini alirudi kuongoza sekretariati mpya chini ya Rais Magufuli na juzi, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete hapa Dodoma, ilidhihirika kuwa Kinana bado yupo yupo sana, angalau mpaka mwaka 2022.

Rais Magufuli alimuomba Kinana kuendelea kushika nafasi yake wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM na kusema ni kutokana na kumsaidia sana katika utendaji kazi wake.

Rais Magufuli alisema amempendekeza Kinana kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa CCM kwa sababu humsaidia kufanya mambo ya mageuzi ndani ya chama hicho na kwamba ni mategemeo yake ataendelea kumsaidia sana kwa kuendelea kushika wadhifa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa Julai 18, mwaka jana, Msemaji wa CCM wakati huo, Christopher Ole Sendeka, alisema kujiuzulu kwa Kinana ni utamaduni uliojengeka ndani ya chama hicho.

“Hili ni suala la utamaduni kwa sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya Mwenyekiti wa chama kupitishwa,” alisema Ole Sendeka. “Ni utamaduni kwa sekretarieti kupisha na kumpa nafasi mwenyekiti mpya wa chama kuunda safu yake ya utendaji ya chama.”

Alibainisha Kinana kwa niaba ya sekretarieti nzima angekabidhi barua kwa mwenyekiti huyo ili yeye na sekretarieti hiyo waweze kumpisha Rais Magufuli kupanga safu yake.

“Kama atapenda, amrejeshe atakayependa kumrejesha, atakayetaka kufanya naye kazi kwa kadri itakavyompendeza… mwenyekiti mpya ataamua,” alisema Ole Sendeka siku hiyo.

Alisema utamaduni huo hufanywa ili mwenyekiti aweze kupata timu ya kufanya nayo kazi ambayo itakidhi matarajio yake, katika kuleta maendeleo na mabadiliko ndani ya chama chenyewe.

Utaratibu wa kuachiana kiti CCM ulianzia kwa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipomaliza muda wake mwaka 1995, na hivyo kukabidhi nafasi ya Mwenyekiti kwa Benjamin Mkapa 1996 ambaye alifanya hivyo pia kwa Kikwete mwaka 2006.

Rais Magufuli alimteua Kinana na sekretarieti yake kuendelea na kazi zao baada ya kuchaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa tano wa CCM siku tano baadaye.

Akisoma taarifa ya utekelezaji wa chama kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita jana, Kinana alimshukuru Rais Magufuli kwa kumchagua kuendelea naye.

“Nakushukuru kwa kuendelea kuniamini na kukubali utendaji kazi wangu,” alisema Kinana. “Nitafanya kazi kwa bidii, maarifa na kwa uaminifu mkubwa.

“Haiwezekani kumkatalia mwenyekiti wako na Rais wako, imani huzaa imani na uhakika umenitaka niendelee kuchapa kazi ndani ya chama chetu.”

Alisema kwa kuwa ana imani na uwezo wa kufanya kazi vizuri na kwamba kauli ya Mwenyekiti ni maagizo hivyo kumhakikishia atakitumikia chama kwa bidii na uaminifu.

Alisema Mwenyekiti Magufuli amempa uhuru katika baadhi ya maeneo.

MZEE MUGABEMwenyekiti wa CCM Magufuli pia alielezea shukrani zake kwa msaada mkubwa katika uongozi anaopata kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na wa Zanzibar, Alli Mohammed Shein.

“Hawa makamu wawili wamenisaidia sana,” alisema Mwenyekiti Magufuli na kubainisha “kuna watu walijua sitamchagua Mangula”.

“Wengine walikuwa wanamuita huyu mzee ni Mugabe.

“Hakuna kazi ya kukitumikia chama bila kutegemea wazee… ni muhimu sana busara zao zinahitajika sana.”Alisema makamu hao wamemsaidia sana maana kwa kuwa yeye ni kijana, wakati mwingine huwa “nachemka” lakini Shein na Mangula wamemsaidia kumfanya awe kiongozi mzuri.

Akizungumza baadaye mkutanoni humo, Katibu Mkuu Kinana alisema baadhi ya watu wamekuwa wakibadilisha mageuzi yaliyofanywa na chama hicho kwa lengo la kumchafua mwenyekiti wake.

“Wapo wanaosema kuwa tumebadilisha katiba (ya chama) na kwamba Rais Magufuli atakapomaliza kipindi cha miaka mitano hakuna wa kumpinga. Ataendelea tu,” alisema na kufafanua:

“Mimi sijawahi kuona hiyo, wala kwenye mageuzi hayapo, lakini hiyo yote ni kutaka kumchafua mwenyekiti.”Lazima tukatae, msiyakubali.”

Kinana alisema katika awamu zote Serikali zilikuwa zikipambana na rushwa, lakini tofauti yake ni kwamba kwa awamu ya tano hatua kali zinachukuliwa hapo hapo.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here