SHARE

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Siha ambaye pia ni diwani wa Gararagua, Zakaria Lukumay amejiuzulu uanachama wa (Chadema) na kujiunga na CCM.

Lukumay ametangaza kujiuzulu siku kadhaa baada ya aliyekuwa mbunge wa Siha (Chadema), Dk Godwin Mollel kujivua ubunge na kujiunga na CCM.

Sawa na Dk Mollel, diwani huyo amesema uamuzi wake unatokana na kumuunga mkono Rais John Magufuli katika kutetea na kulinda rasilimali za Taifa.

Katika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha inayoonyesha iliandikwa Desemba 24,2017 Lukumay amesema anajiunga na CCM kwa sababu ndicho chama kinachogusa mahitaji ya Watanzania wote.

Aliyekuwa diwani wa Chadema wa Donyomurwak wilayani Siha, Lwite Ndossi maarufu Nsonuu Desemba 19,2017 alijivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM.

Taarifa iliyotolewa na idara ya itikadi na uenezi ya CCM Desemba 19,2017 ilisema Ndossi alieleza sababu za kujiunga na CCM ni kuwa amejiunga na watu wanaofanya siasa za kufanya kazi za maendeleo na si kulumbana na maneno matupu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here