SHARE

Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeidhinisha gawio la Sh300 bilioni kwa Serikali kutokana na faida iliyopatikana kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Kiasi hicho kinafanya jumla ya gawio la BoT katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2014/15 hadi 2016/17 kuwa Sh780 bilioni.

Taarifa ya BoT iliyotolewa  kwa vyombo vya habari imesema mwaka 2014/15 ilitoa gawio la Sh180 bilioni na mwaka 2015/16 lilikuwa Sh300 bilioni.

Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu katika taarifa hiyo amesema kifungu cha 18 (5) cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kinaipa BoT mamlaka ya kutoa gawio kwa Serikali pale inapotengeneza faida.

“Majukumu ya msingi ya Benki Kuu si kutengeneza faida; hata hivyo, inapotokea kwamba faida imepatikana, sehemu kubwa hutolewa kama gawio kwa Serikali,” amesema Profesa Ndulu katika taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, amesema jukumu la msingi la Benki Kuu ya Tanzania ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kujenga mfumo wa fedha ulio imara na unaofaa kwa ukuaji endelevu wa uchumi wa Taifa.

Majukumu mengine ni kuchapisha noti na sarafu za Shilingi ya Tanzania; usimamizi wa mabenki na taasisi za fedha; kusimamia na kudhibiti mifumo ya malipo ya Taifa; kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni ya Taifa; kutoa ushauri wa kiuchumi na fedha kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; ni Benki ya Serikali hizo na taasisi zake, na ni benki ya mabenki.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here