SHARE

ALIYEKUWA Rais wa Zimbabwe na kuondolewa madarakani hivi karibuni, Robert Mugabe, amepatiwa mafao kibao ya kustaafu ambayo hutolewa na na serikali kwa viongozi wastaafu. Miongoni mwa marupurupu yake ni pamoja na kupewa wasaidizi 20, usafiri wa ndege na magari mbalimbali ya kumhudumia.

Hayo yamekuja baada ya kiongozi huyo kuachia madaraka ambapo iliripotiwa kwamba pamoja na marupurupu mengine, angepewa bonasi ya Dola milioni 10 (sawa na Sh. bilioni 22) Marupurupu hayo yalitangazwa Jumatano wiki hii na Rais Emmerson Mnangagwa ambapo watumishi wote 20 wa Mugabe wakiwemo walinzi sita, na gharama zote za magari ya kifahari atakayopewa, yakiwemo aina ya Mercedes Benz S500, yatagharimiwa na serikali.

Isitoshe, Mugabe na mke wake watapatiwa pasipoti za kibalozi. Vilevile, wamepewa fursa ya kusafiri kwa ndege mara nne kwa mwaka ndani na nje ya Zimbabwe kwa kutumia daraja la kwanza. Watapewa pia makazi mahali popote katika Jiji la Harare, ambapo samani na zana zote zinazohitajika na fedha za viburudisho zitalipwa na serikali.

Mugabe ambaye alijiuzulu Novemba 21 mwaka huu baada ya chama chake kumfukuza na kuanza hatua za kumfungulia mashitaka, amehakikishiwa pia kupata bima ya matibabu, mkewe na wategemezi wake wote. Utawala wake uliochukua miaka 37 ulidaiwa kujaa uvunjaji wa haki za binadamu, wizi wa kura na kuporomoka kwa uchumi hadi pale Mnangawa alipochukua hatamu za uongozi. Hiyo ni baada ya Mugabe kuungana na mkewe Grace (52) katika shutuma za kumpiga vita Mnangagwa.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here