SHARE

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amewatembelea walinda amani wa Tanzania, waliojeruhiwa wakiwa kazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika shambulio, lililosababisha vifo vya wapiganaji 15 wa Tanzania na kujeruhi wengine 44 waliopo chini ya mwamvuli wa majeshi ya Umoja wa Mataifa (MUNOSCO).

Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), aliwatembelea askari hao katika Hospitali ya Nakasero jijini Kampala, wanakoendelea na matibabu baada ya shambulio hilo la Desemba 8, mwaka huu huko Kivu Kaskazini, DRC.

Akiwa katika Hospitali ya Nakasero, alikozungumza na wapiganaji hao na kuwataka kutorudi nyuma, Rais Museveni alipokelewa na Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda, Brigedia Jenerali Skilder Makona.

Rais Museveni alilaani shambulio hilo.

Madaktari hospitalini hapo walimhakikisha Rais Museveni kuwa wapiganaji hao hawapo katika hali mbaya na kwamba watarejea katika hali ya kawaida hivi karibuni. Naye Brigedia Jenerali Makona alimshukuru Rais Museveni kwa ushirikiano wake na kitendo cha kutenga muda kwenda kuwajulia hali wapiganaji hao hospitalini.

Wakati Rais Museveni akiwafariji wapiganaji hao wa Tanzania, Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF) limesema limewaua wapiganaji 100 wa kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) baada ya mapambano makali hivi karibuni huko Mashariki mwa DRC.

Walitumia ndege za kivita na silaha nyingine, kushambulia kambi za waasi hao wanaioshi katika kambi nane katika eneo la Eringeti ambazo zote zimeteketezwa. Kwa mujibu wa msemaji wa operesheni hiyo, Meja Ronald Kakurungu aliyezungumza kwa simu kutoka mpaka wa magharibi katika wilaya ya Bundibugyo, wapiganaji wa UPDF walivamia kambi za ADF za Madina, Canada, Tadia, Popoke, Makayoba, Kainama, Ngiti na Kikingi baada ya taarifa za kiintelijensia kuvuja zikieleza kuwa waasi wanajiandaa kuishambulia Uganda.

Askari wa JWTZ Kwa mujibu wa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa askari 14 waliouawa siku ya shambulio, walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano baina yao yalidumu kwa saa 13.

Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 walijeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo. Baadaye, majeruhi mmoja alifikwa na mauti na hivyo kufanya idadi ya vifo vya wapiganaji hao kufikia 15.

Mwakibolwa alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu. Alikiri kuwa, shambulio hilo ni kubwa zaidi kutokea tangu JWTZ ianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011.

Hata hivyo, alisisitiza tukio hilo halitawavunja moyo JWTZ wala kutetereka kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi, bali linawaongezea ari, nguvu, ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu yao. “Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC.

Kwa umoja wetu Watanzania tuwaombee dua roho zao zipumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao,” alisema Luteni Jenerali Mwakibolwa.

Mbali ya taarifa za vifo vya askari hao kuwashitukia Watanzania wakiongozwa na Rais, Dk John Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, pia Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Katibu Mkuu wake, Antonio Guterres ulishutumu shambulio hilo na kusema ni sawa na uhalifu wa kivita. Guterres alisema shambulio hilo ndilo baya zaidi, kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here