SHARE

UPEPO umebadilika. Nyota mpya wa Simba, Asante Kwasi amebadili upepo ndani ya klabu hiyo baada ya kuchukua majukumu ya wachezaji watatu uwanjani katika mchezo wake wa kwanza tu tangu atue Msimbazi katika dirisha dogo la usajili.

Kwasi aliyejiunga na Simba akitokea Lipuli ya Iringa, aliichezea timu hiyo kwa mara ya kwanza juzi Alhamisi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kufunga bao moja katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Pemba.

Katika mchezo huo, Kwasi alianza sambamba na Juuko Murshid jambo lililoashiria mabeki waliokuwa wakicheza kwenye nafasi hiyo wanatakiwa kujipanga upya.

Nafasi hiyo awali ilikuwa ikichezwa na Yusuf Mlipili na James Kotei ambaye hata hivyo amerejeshwa kwenye nafasi yake ya kiungo.

Kama hiyo haitoshi, Kwasi alichukua majukumu ya kupiga mipira ya adhabu kazi iliyokuwa ikifanywa na Shiza Kichuya. Kwasi alipiga mipira yote ya adhabu katika mchezo huo.

Beki huyo wa zamani wa Mbao FC pia alichukua jukumu la mipira ya kurusha hasa katika eneo la adui na urushaji wake ulionekana kuwa kama mpira wa kona.

Kwasi anafuata nyayo za Fred Mbuna na Mbuyu Twite waliokuwa wakisifika vikali kwa mipira hiyo ya kurusha.

Beki huyo pia alionyesha kiwango cha juu katika kukaba, kupandisha timu, pia kufanikiwa kufunga. Muda mwingi wa mchezo alifanya kazi ya kuhamasisha timu majukumu ambayo mara nyingi hufanywa na nahodha.

Akizungumza na gazeti la  Mwanaspoti, Kwasi alisema “Nashukuru nimeanza vizuri, siwezi kuzungumza mengi kwa kuwa utaratibu wa hapa unanitaka nipate kwanza ruhusa kwa meneja, ila nashukuru sana.”

Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe alisema Kwasi ameonyesha mwanga katika mechi yake ya kwanza lakini anatakiwa kujituma zaidi ili kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza na kuibeba timu yake.

“Ni mchezaji mzuri, amefanya vizuri tangu akiwa Mbao na Lipuli. Tofauti kwa sasa, anacheza Simba ambayo ni timu kubwa, anatakiwa kufahamu hilo,” alisema Ulimboka aliyeshinda mataji matano ya Ligi Kuu na Simba.

“Ameanza vizuri ila anaweza kufanya vizuri zaidi. Kikubwa ni kucheza kwa ushirikiano mkubwa sambamba na wachezaji wenzake, wacheze kwa mshikamano pia.

“Anaweza kuongeza hamasa ndani ya timu pia, nimeona kuna wakati anakuwa kama kiongozi. Anachangamsha timu na anasaidia kwenye kushambulia,” alisema Ulimboka.

“Akipata muda mwingi wa kucheza kwenye Ligi anaweza kuongeza kiwango chake zaidi. Nafasi ya beki ya kati sasa ina ushindani mkubwa, hivyo kocha atakuwa akimpa nafasi mchezaji mwenye makosa machache.”

Mrundi apata dawa ya mabao

Katika hatua nyingine, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Masudi Djuma ameipata dawa ya mabao ya timu yake, huku akiwaambia nyota wake kuwa kazi ya kufunga ni ya kila mmoja na sio mastraika pakee yao.

Kocha huyo ameanza vizuri kibarua chake Msimbazi akiwa hajapoteza mchezo wowote katika mechi tatu alizokaa benchi.

Juzi Alhamisi aliiongoza Simba kupata ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Jamhuri ya Pemba.

Kauli hiyo ya Djuma imekuja siku moja baada ya beki mpya wa Simba, Asante Kwasi kuifungia timu hiyo bao moja katika mchezo wake wa kwanza tu klabuni hapo.

“Kwasi amefunga na ni mchezaji mzuri ila nataka kila mchezaji ndani ya timu yangu afunge, bila kujali anacheza nafasi gani. Naamini wengi watafunga tu, ukiachana na washambuliaji ambao ndiyo kazi yao,” alisema Djuma.

Akimzungumzia straika Mrundi, Laudit Mavugo ambaye alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza hapo juzi, Djuma alisema;

“Mavugo bado hayupo fiti lakini ni lazima acheze ili aendelee kuwa imara, vinginevyo nitakuwa simsaidii kurudisha kiwango chake cha awali.”


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here