SHARE

Katika kile kinachoonekana kuwa kila zama na kitabu chake, familia ya rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe iliyoishi maisha ya kifahari sasa inakabiliwa na uwezekano mkubwa wa kukamatwa.

Tayari Tume ya Kupambana na Rushwa ya Zimbabwe (ZACC) imeanza wiki hii kuwachunguza watoto wa Mugabe; Bellarmine Chatunga na Robert Junior, pamoja na mtoto wa kambo Russell Goreraza, mkwewe Simba Chikore na wanasiasa kadhaa waliopata kuwa mashuhuri kwa makosa kuanzia ya biashara haramu ya dhahabu, matumizi mabaya ya ofisi, ufisadi na mauaji.

Uchunguzi huu unafanywa na Serikali ya Rais Emmerson Mnangagwa ambaye alianzisha kampeni za kukabiliana na ufisadi na hadi sasa imewafungulia mashtaka aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani Ignatius Chombo kwa kujihusisha na ufisadi, waziri wa zamani wa madini Walter Chidhakwa, waziri wa zamani wa kilimo na umwagiliaji Joseph Made.

Taarifa zilizoenea ni kwamba mawaziri kadhaa wa zamani, makatibu na watu wa familia ya Mugabe huenda wakakamatwa.

Mnangagwa aliwataka mawaziri waliotuhumiwa kwa ufisadi wajitokeze kujisafisha na wasalimishe mali walizopata kifisadi.

Katika mfululizo wa mapambano dhidi ya rushwa, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe (UZ) Levi Nyagura huenda akakamatwa kutokana na uamuzi wa chuo wa kumtunukia shahada ya uzamivu (PhD) Grace Mugabe kinyume na taratibu mwaka 2014.

Habari kutoka ndani ya ZACC zinasema kikundi cha wahadhiri wapatao 15 kimeandika barua kikieleza kwamba UZ ilikiuka taratibu zilizopo hadi kufikia kumtunuku shahada Grace.

“Uchunguzi dhidi ya Nyagura umekamilika; atakamatwa wakati wowote. Ukweli kukamatwa kwake kumeahirishwa kumpa fursa Rais kukutana na makamu wa vyuo vikuu na vya ufundi wiki ijayo,” limeandika gazeti la New Zimbabwe.

“Katika wiki chache zijazo mtashuhudia baadhi ya mawaziri wakisalimisha mali zao kimya kimya hasa majengo kwa kisingizio wanazipatia jamii na kuwapa uwezo maskini. Ikiwa (mawaziri) hawatafanya hivyo kwa hiari, basi wataaibishwa nguvu itakapotumika. Ikiwa watakataa kutii amri watachunguzwa na kushtakiwa,” alisema ofisa wa ngazi ya juu.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here