SHARE

Hali ya mshangao imetawala kwa mawaziri wa Kenya ambao hawakutajwa kwenye baraza jipya la mawaziri la Rais Uhuru Kenyatta alilolitangaza Ijumaa iliyopita lililowaacha nje ya ofisi zao mawaziri sita aliokuwa nao kwenye awamu yake ya kwanza.

Baada ya kuapishwa, Rais Kenyatta ameanza kuunda Serikali kwa kutangaza baraza lake akiwateua mawaziri watatu wapya na kuwaacha wengine sita waliokuwapo awali.

Mawaziri wa zamani walioachwa kwenye nafasi zao ni pamoja na Fred Matiang’i (Mambo ya Ndani), Charles Keter (Nishati), Najib Balala (Utalii), Henry Rotich (Fedha), Joe Mucheru (Tehama) na James Macharia (Uchukuzi).

Hata hivyo, hatima ya mawaziri wengine ambao hawakutajwa bado haijajulikana licha ya kwamba wanaendelea kushika ofisi zao mpaka pale Rais Kenyatta atakapotangaza mawaziri wapya au kuwaacha wenyewe.

Baadhi ya mawaziri na wasaidizi wao wamekataa kukubali kwamba wameondolewa kwenye wizara zao wakisisitiza kwamba bado wanashikilia nafasi kwa sababu baraza zima la mawaziri bado halijakamilika.

“Rais hajanifukuza mimi, ametaja tu baadhi ya mawaziri ambao anapenda wabaki kwenye nafasi zao na kuteua wengine wachache. Mpaka mchakato wote utakapokamilika, huwezi ukasema amenifukuza. Naweza kupelekwa kwenye nafasi nyingine unajua,” alisema waziri mmoja ambaye si mmoja kati ya sita waliotajwa na Rais Kenyatta.

Ijumaa iliyopita Rais Kenyatta alitangaza mawaziri wapya watatu na kuwabakiza wengine sita kwenye nafasi zao.

“Napenda kutangaza kwamba ninawaacha watu wafuatao kwenye baraza langu la mawaziri na nitawapangia majukumu yao tena kwa mujibu wa Ibara ya 152(5)(A) ya Katiba na watu hao ni Fred Matiang’i (Mambo ya Ndani), Charles Keter (Nishati), Najib Balala (Utalii), Henry Rotich (Fedha), Joe Mucheru (Tehama) na James Macharia (Uchukuzi),” alisema Rais Kenyatta.

Juzi, kitu ambacho kinaweza kutafsiriwa kama kuwapunguzia msongo wa mawazo mawaziri ambao hawakutajwa, msemaji wa Ikulu ya Kenya, Manoah Esipisu alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema mawaziri wote bado wanashikilia nafasi zao mpaka pale mchakato wa kuunda baraza la mawaziri utakapokamilika.

Taarifa hiyo ya Esipisu ilikuwa ikimaanisha kwamba mpaka sasa hakuna waziri ambaye amefukuzwa kazi na Rais Kenyatta.

“Hii ni kufafanua kwamba mawaziri wote ambao bado wako ofisini wataendelea kutambulika kama ilivyoelekezwa kwenye waraka wa mkuu wa utumishi wa umma Desemba mwaka jana, mpaka hapo itakapoamriwa vinginevyo,” alisema Esipisu katika taarifa hiyo.

“Siku zijazo, Rais Kenyatta atahitimisha kazi yake ya kuunda timu ya ofisi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na wanaoipenda kazi yao ya kuwahudumia wananchi kwa kufuata katiba.”

Kwa mujibu wa vyanzo viwili vya habari kutoka ndani ya Ikulu ya Kenya vimeliambia gazeti la The Standard kwamba, Rais Kenyatta amekuwa akifanya mambo yake kwa usiri na ulinzi mkubwa.

“Sikiliza, ngoja nikwambie. Serikali haifukuzi watu, inaondoa majina yao kwenye orodha ya wateule wa Rais. Nina uhakika mlishaliona hilo siku zilizopita. Kwa hiyo kama ndugu yake ametaarifiwa rasmi kwamba anataki kwenye baraza, nini kimebakia kwa mawaziri ambao bado wako ofisini?” kilisema chanzo kimoja cha habari.

Hata hivyo, msimamo huo ulitofautiana na chanzo kingine cha habari kutoka serikalini ambacho kilisema baadhi ya mawaziri ambao hawakutajwa Ijumaa akiwamo Eugene Wamalwa, Amina Mohammed, Mwangi Kiunjuri na Dan Kazungu wamefanya vizuri katika ofisi zao na kwamba wanaweza kubaki kwenye baraza la mawaziri.

“Kuna uwezekano baraza la mawaziri likaongezeka. Mawaziri sita waliotajwa na Rais wataendelea na nafasi zao isipokuwa Matiang’I ambaye anakwenda Wizara ya Mambo ya Ndani. Hiyo haimaanishi kwamba wale ambao hawakutajwa na Rais basi wamefukuzwa kazi,” kilisema chanzo hicho.

“Ina maana kwamba watu kama Amina, Eugene, Adan Mohammed, Kiunjuri and Kazungu watarudi lakini si lazima warudi kwenye nafasi wanazozishikilia sasa. Kwa kifupi ni kwamba mawaziri sita tu ndiyo wanajua nafasi zao.”

Rais Kenyatta na makamu wake, William Ruto wameweka usiri mkubwa katika chaguo la wateule kiasi kwamba hata wasaidizi wao wa karibu hawajui kitu.

Inafahamika wazi kwamba maofisa wa ngazi za juu waliokuwapo Ikulu wakati Rais Kenyatta akitangaza mabadiliko hayo hawakujua alikwenda kuzungumzia nini. Walijua atakwenda kuzungumzia mabadiliko kwenye sekta ya elimu.

Rais ameachana pia na utaratibu wa zamani ambao teuzi zake zilizingatia ukarimu, ukanda na urafiki. Si rahisi kwa sasa kutabiri nafasi chache za uteuzi zilizobaki.

Sambamba na hilo, Rais alifanya uteuzi wa kushtukiza kwa kumteua mkuu wa Mkoa wa Rift Valley, Wanyama Musiambo kuwa naibu mkuu wa utumishi wa umma akimaliza tetesi za watu waliotajwa kuchukua nafasi hiyo ambao ni Makati Wakuu Joseph Njoroge (Nishati), Karanja Kibicho (Mambo ya Ndani) na Monica Juma (Mambo ya Nje).

Watu wengi walitarajia Amina, Kiunjuri, Wamalwa na Kazungu kuachwa kwenye nafasi zao kwa sababu ni wanasiasa hodari na wachapakazi na walikuwa na mchango mkubwa kwa Kenyatta kuchaguliwa katika muhula wake wa pili.


LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here